Binti Miaka 19 Awa Gumzo Kazi ya Mochwari
Sabrina Gharib, binti mwenye miaka 19 anayefanya kazi kwa vitendo kimasomo kwenye Mochwari ya Hospitali ya Rufaa ya Tumbi Kibaha mkoani Pwani, amekuwa gumzo kwa watu wanaokwenda kuchukua miili ya wapendwa wao hospitalini hapo, Uwazi limeibuka naye.
“Tulipokwenda kuchukua mwili wa mpendwa wetu Tumbi, tulisikia watu wakimzungumzia msichana mdogo anayehudumia maiti. Kwanza sikuamini lakini nilimuona na kwa kweli alituhudumia vizuri,” alisema Frida John, mmoja wa waliokwenda kuchukua maiti hospitalini hapo.
Katikati ya wiki iliyopita, gazeti hili lilikwenda hospitalini hapo likiwa na kundi zima la Global Tv On Line na kufanya mahojiano naye ambapo Sabrina alisema aliamua kusomea kazi ya kuhudumia maiti badala ya unesi kutokana na kujua kuwa, ajira kwa fani hiyo zipo nje nje.
MSIKIE MWENYEWE
“Niliamua kusomea kazi hii kwa kujua kuwa ina soko la ajira. Awali nilikuwa msichana pekee darasani. Siku ya kwanza kusoma kwa vitendo katika Hospitali ya Iringa, nililia kwa sababu niliona kama maiti naiumiza lakini mwalimu wangu aliniambia nisiwe na hofu, mtu huyo amekwishafariki dunia, hivyo hasikii maumivu,” alisema Sabrina.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Shirika la Elimu Kibaha, Pwani ambao ndiyo wamiliki wa Hospitali ya Tumbi, Lucy Semindu, akimuelezea msichana huyo alisema ni jasiri ambaye amefanya kazi nzuri wakati wa elimu yake kwa vitendo.
“Ameonesha mfano mzuri na kuthibitisha kuwa wanawake wanaweza,” alisema Lucy.
Naye mmoja wa viongozi katika mochwari hiyo ya Tumbi, Francis Kobelo alisema msichana huyo ni mfano wa kuigwa.
“Ukimwambia fanya hivi, hana hofu, anafanya, inaweza kuja maiti imeharibika ukimwambia fanya moja, mbili, tatu na baadaye ukija kuikagua unakuta amefanya vizuri sana,” alisema Kobelo.
Mama mzazi wa Sabrina, Asha Ramadhani alipohojiwa alisema siku ya kwanza alipopigiwa simu na binti yake huyo kumwambia anachukua masomo ya kuhudumia maiti mochwari, alichanganyikiwa.
“Nilimuuliza unataka kuwa chizi? Lakini sikuwa na la kufanya, nilimuacha aendelee na masomo yake,” alisema mama huyo huku akibainisha kuwa, Sabrina ni mwanaye wa kwanza.
Chanzo: GPL