CUF Yapata Pigo Jingine
Chama Cha Wananchi (CUF) upande wa Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad kmepata pigo jingine kufuatia Mahakama Kuu nchini Tanzania kutupilia mbali pingamizi lao kutaka Profesa Ibrahim Lipumba asipewe ruzuku za chama hicho.
Mahakama Kuu imetupilia mbali pingamizi hilo leo tarehe 11 Agosti 2017, kufuatia Chama Cha CUF huko nyuma kufungua kesi ya msingi ya madai kuhusu wizi wa ruzuku na shauri dogo la kuweka zuio kutolewa kwa ruzuku ya chama kutokana na wizi wa shilingi milioni 369 ambazo zilidaiwa kuibwa na Lipumba na kundi lake kwa kushirikiana na Msajili wa Vyama Vya Siasa.
Pingamizi hilo limedumu kwa miezi minne kutoka Machi mwaka huu mpaka Agosti ambapo leo Mahakama Kuu imetupilia mbali zuio hilo lililowekwa na CUF upande wa Katibu Mkuu, hali ambayo inapelekea Msajili wa Vyama vya Siasa kuendelea kutoa ruzuku ya Chama hicho kwa Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Msajili wa Vyama Vya Siasa nchini Profesa. Ibrahi Lipumba na wananchama wake ambao wanamuunga mkono.
Toka mwezi wa Septemba 24, 2016 baada ya Profesa Lipumba kudaiwa kufanya uvamizi wa ofisi za chama cha CUF pale Buguruni kinyume na sheria na taratibu baada ya Kujiuzulu kwa hiari yake na kuiacha ofisi hiyo takribani kwa kipindi cha mwaka mzima ndipo ulipoanza mgogoro kati ya pande mbili, upande unaomuunga mkono Lipumba na upande unaomuunga mkono Maarim Seif jambo ambalo limesababisha madhara mengi ya moja kwa moja ndani ya chama hicho.