-->

Filamu Zetu Zinapotushawishi ‘Tunywe Maji Mengi’

NAWASALIMU wapendwa wasomaji wa gazeti hili, hasa katika kipande hiki ambacho kinatupa wasaa za kuzungumzia masuala kadha wa kadha katika nyanja ya filamu hapa nchini.

Ray

Ray

Nimekuwa nikiandika mambo mengi katika eneo hili na kwa hakika baadhi ya wadau wamekuwa na mrejesho mzuri kuhusu mada ninazoziandika. Yapo mengi ambayo yanaendelea kwenye filamu zetu na nimekuwa nikiyaeleza mazuri na mengine yale yenye changamoto.

Leo katika makala yangu naangalia suala moja ambalo kwa sasa limekuwa kawaida kabisa kwa wasanii wetu wa kike na kiume. Hili linaweza kuwa baya na bila shaka halitawapendeza wengi, lakini ni muhimu sana tukalijadili kwa sababu lina madhara makubwa.

Bila shaka katika kipindi hiki cha wiki mbili gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu sanaa ni ile hali ya ‘kunywa maji mengi’ iliyoibuliwa na msanii nguli wa filamu hapa nchini, Vincent Kigosi, maarufu kama Ray.

Kunywa maji mengi imekuwa ni tafsiri ya kutafuta weupe, lakini kimsingi mada hiyo imekuwa gumzo kwa sababu watu wengi wamepingana na kauli ya Ray. Hakuna ubishi na inafahamika kwamba baadhi ya wasanii wetu wa filamu wamekuwa na tabia ya ‘kujikrimu’ kwa maana ya kubadilisha mwonekano wa ngozi zao ili wawe weupe.

Wasanii wetu wengi hivi sasa wanajichubua kama wenyewe tulivyozoea kusema, wanataka kuwa weupe na mbaya zaidi hali hii imekuwa wa wasanii wa jinsi zote na sasa imekuwa kama ndiyo mtindo, kwani wengi sasa wanafanya shughuli hiyo.

Kwani ukiwa mweusi huwezi kuigiza vizuri?  Au kuigiza kwa rangi tulizonazo ambazo tumepewa na Mwenyezi Mungu kwenye filamu tutawatisha watazamaji? Haya ni baadhi tu ya maswali ambayo nimekuwa nikijiuliza kila ninapoona filamu za baadhi ya wasanii wetu.

Sasa imekuwa zaidi ya kujichubua, bali kwa vijana wa kiume ni kutafuta urembo, sizungumzii urembo wa kawaida ambao utasaidia kufanya picha zitoke nzuri, bali wasanii wetu sasa wanataka urembo wa kuonekana hata nje ya kamera, ndiyo hivyo sasa wanajichubua kabisa rangi za miili yao.

Siku hizi siyo ajabu kuona filamu mbili zimeigizwa na mtu mmoja mwenye rangi mbili, kwa maana kwamba filamu ya mwezi jana alikuwa mweusi lakini ya mwezi huu, ni mweupe kushinda mzungu!

Nilitegemea wasanii kuwa mstari wa mbele kukemea suala hilo, lakini utakuta msanii amechubua ngozi yake hadi mishipa ya damu inaonekana. Mbaya zaidi huo mkorogo haupitishwi pote. Unakuta mtu usoni mkorogo umekolea kwelikweli, lakini shingoni kwake ni kama amejizunguushia kaniki.

Mimi naamini kuwa msanii ni mwalimu nambari moja wa jamiii. Watu wengi wanafanya mambo kwa kuwaiga wasanii. Sasa napata shida ninapoona wasanii vijana wa kiume wanakimbilia kuweka dawa kwenye nywele, kutoga masikio na kujichumbua, maarufu kwa sasa kama kunywa maji mengi.

Ni vyema kuepukana na ulimbukeni huu, kwa wasanii ni busara wakawa walinzi wa maadili ya taifa letu kwa kuepuka kufanya mambo ambayo yanaweza kusababisha janga kubwa kwenye jamii. Tunafahamu kwamba kujichubua kunaweza kusababisha kansa ya ngozi, sasa je, wasanii wetu wanaonyesha mfano gani katika hili?

Haipendezi, tutafakari mara mbili, kwani kadri siku zinavyokwenda wale weusi watadhani kwamba kuwa mweupe ni nyongeza ya kuigiza filamu. Tujadiliane na tuelimishane kunusuru hali hii isiendelee kwa wengine na walioanza waache.

Mtanzania

Comments

comments

Post Tagged with

Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364