Harmonize: ‘Bado’ ni Hisia za Kweli za Diamond
Msanii Harmonize ameelezea jinsi ilivyokuwa kabla hajarekodi wimbo wa bado, na kusema kuwa hakuwahi kuwaza kichwani mwake kuwa wimbo huo ataimba na Diamond.
Akiongea kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, Harmonize amesema ingawa alijua kuwa kuna kazi watafanya wote lakini hakujua kuwa itakuwa ni lini na ni wimbo upi.
“Before wakati naandika nilikuwa siwazi kama ntafanya na Diamond japokuwa tulishakubaliana kuwa tutafanya kazi ya pamoja, kwa sababu tunakuwa tupo na stori pamoja, lakini pia nilikuwa natamani sana kufanya nyimbo na diamond kwa sababu nilikuwa najua itanisaidia kwa sababu muziki wake sehemu nyingi umefika, mi bado, kwa hiyo watanijua kupitia diamond, japokuwa hatukupanga kuwa itakuwa ni katika bado”, alisema Harmonize.
Harmonize aliendelea kwa kusema kuwa baada ya hapo alimtumia wimbo Diamond, na alipousikia alitaka aingize maneno yake, ambayo ameeleza kuwa ni hisia zake za maumivu.
“Wakati naandika nikafanya verse yangu na chorus, alikuwa yupo amerika nikamtumia, akaniambia wimbo ni mkali sana, mi mwenyewe nina maumivu yangu ya kimapenzi, nikiweka humu itakuwa vizuri zaidi, alivyorudi akaniimbia verse ashaandika tayari, nikaona verse ni nzuri tukaanza kutafuta beat”, alisema Harmonize.
Harmonize alimaliza kwa kusema kuwa wimbo huo ni wimbo ambao atauheshimu milele kwa sababu umemtoa katika hatua moja na kumpeleka hatua nyingine ambayo alikuwa hawazi kama ataweza kufika.
eatv.tv