-->

‘Home Coming’ Iwe Fundisho kwa Wasanii Bongo

KATIKA tasnia ya filamu hapa nchini tunaanza kupiga hatua kwa kiasi kikubwa sana kutokana na wasanii wengi kujituma kwa lengo la kutangaza kazi zao ndani na nje ya nchi, huku ikiwa njia mojawapo ya kujipatia kipato.

Baadhi ya wasanii waliojitokeza juzi kwenye uzinduzi wa filamu hiyo MlimaniCity jijini Dar-es-salaam.

Baadhi ya wasanii waliojitokeza juzi kwenye uzinduzi wa filamu hiyo MlimaniCity jijini Dar-es-salaam.

Siku zote tumekuwa tukiona filamu zetu za hapa ndani zikitazamwa kwa muda mfupi na zinaanza kusahaulika kutokana na uwezo mdogo wa wasanii kufanya filamu hiyo na kutokuwa na ubunifu wa kutosha.

Kwa sasa kumekua na tabia ya kuangalia filamu za nje ya nchi kama vile Nigeria, Marekani na nchi nyingine mbalimbali kutokana na ubunifu wa wasanii hao wa nje.

Kumbe kwa hapa Tanzania inawezekana kufikia hatua hiyo kama wasanii wenyewe watakuwa wanajituma na kuwa na ubunifu, endapo wasanii watafanya hivyo basi itakuwa ni kazi rahisi kuanza kuzisahau filamu za nje ya nchi.

Wakati wa marehemu Steven Kanumba, tulianza kusema kwamba filamu zetu zinaanza kuvuka mipaka kwa kuwa alikuwa mbunifu wa hali ya juu na alikuwa na uwezo wa kucheza filamu kutokana na uhalisia wa filamu hiyo.

Msanii huyo aliweza kuwashusha baadhi ya wasanii mbalimbali wakubwa kutoka nje ya nchi kama vile Nigeria, ambapo alifanikiwa kumleta na kufanya naye kazi Ramsey Noah, mkali wa filamu nchini humo.

Baada ya kifo chake tulianza kusahau ubora wa filamu za Bongo kwa kuwa zilianza kupoteza mvuto wake, hivyo watu walianza kuachana nazo kwa kuwa wasanii wengine walishindwa kutumia nafasi hiyo kuweza kuzifikisha filamu zetu kimataifa zaidi japokuwa kuna wasanii wengi wenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi hiyo.

Lakini kwa sasa tunaanza kurudishwa kule ambako Kanumba alikuwa na lengo la kutaka tufike hasa kimataifa, iko wazi kwamba jambo hilo linawezekana kwa asilimia kubwa endapo wasanii hao wanapewa nafasi.

Kuna baadhi ya filamu hapa nchini kwa sasa ambazo zinafanya vizuri na zinaonesha wazi kwamba kuna wasanii ambao wanataka kuitangaza Tanzania katika mataifa mbalimbali, yapo mataifa ambayo yanatambua uwezo wa nchi hii, lakini kutokana na mfumo uliopo kunatakiwa kuwa na mwonekano wa kisasa zaidi.

Kutokana na hali hiyo, kuna wasanii ambao wameamua kuumiza vichwa vyao kwa ajili ya kufikia hatua ambayo mataifa mengine kama Nigeria yamefikia katika filamu.

Juzi hapa jijini Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa Mlimani City, kulifanyika uzinduzi wa filamu mpya ya ‘Home Coming’, ambayo inaonekana wazi kwamba imekusudia kukata kiu ya mashabiki wa filamu ambao wamekuwa wakizikacha filamu zao na kukimbilia zile za nchi jirani.

Hii ni filamu ambayo imekuja kuteka soko kutokana na ubora wake, imekuwa tofauti sana na filamu ambazo tumezizoea, ninaamini kwamba filamu hii itawafanya wasanii wengine waangaike jinsi ya kutaka kuipita filamu hiyo.

Endapo kama itatokea filamu mpya ambayo itaweza kuupita ubora wa filamu hiyo, basi lazima Tanzania tujivunie kwamba tunaendelea kuvuka mipaka ya kimataifa kwa kuwa tutakuwa tupo juu zaidi ndani na nje ya Tanzania.

Wasanii ambao wamecheza katika filamu hiyo wengine sio wenyeji sana kama tulivyowazoea akina Wema Sepetu, JB, Vicent Kigosi, Kajala na wengine wengi, lakini ndani ya filamu hii wasanii wenye majina makubwa ni Hashim Kambi na Ahamed Olotu, lakini wengine sura zao sio ngeni sana ila sio wakongwe kwenye filamu.

Filamu hiyo ina ujumbe mpana sana ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya ofisi, rushwa, elimu na uhusiano, wakati huo kila mmoja amevaa uhusika wake na ameutendea haki.

Sio filamu ya kukosa kuiangalia ni lazima ujifunze kitu na haichoshi kuitazama kwa kuwa ina mvuto wa hali ya juu, ubunifu na mambo mengine mbalimbali na unaweza kuitazama mtu wa aina yoyote bila ya kujali umri.

Katika uzinduzi wa filamu hiyo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye, ambaye aliambatana na baadhi ya wasanii mbalimbali wa filamu na muziki wa hapa nchini.

Nnauye amesema kuwa kutokana na ubora wa filamu hiyo ni wazi kwamba Tanzania tunazidi kupasua anga za kimataifa na amewataka wasanii kuiga ubora wa filamu hiyo ili kuweza kuitangaza zaidi Tanzania kimataifa.

“Ni wazi kwamba Home Coming ni filamu ambayo Watanzania wengi walikuwa wanahitaji kuona wasanii wao wakifanya hivyo, hii ni filamu moja wapo ya kujivunia ambayo tunaweza kusema lolote katika filamu.

“Wapo wasanii wengi wenye uwezo mkubwa ambao wanaweza kufanya zaidi ya Home Coming, ila wanatakiwa kuwa wabunifu wa hali ya juu na kuonesha uhalisia wa filamu husika.

“Home Coming itatoa fundisho kwa wasanii wengine kuweza kufanya makubwa zaidi ya hapo, kwa kuwa hauwezi kufanya jambo zuri kama halipo zuri zaidi ya hilo, hivyo kutokana na ubora wa filamu hiyo ninaamini wasanii sasa watafanikiwa kufanya filamu bora zaidi ya hapo.

“Nawapongeza wasanii ambao wameitengeneza filamu hiyo, kiukweli wameitendea haki stori hiyo, haichoshi kuitazama,” alisema Nnauye.

Ni wazi kwamba Tanzania tunavuka mipaka ya kimataifa katika tasnia ya filamu, kikubwa ni kuwapa sapoti wasanii wetu ili waweze kufanya vizuri zaidi. Home Coming haichoshi kuitazama.

Mtanzania

Comments

comments

Post Tagged with

Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364