Jide: Ray C Anahitaji Marafiki Sahihi
STAA wa muziki wa Bongo Fleva, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ a.k.a Jide, amesema msanii mwenzake, Rehema Chalamila, anahitaji marafiki sahihi ambao watamsaidia katika kipindi hiki kigumu.
Ray C ambaye amewahi kujihusisha na madawa ya kulevya, kwa sasa ameripotiwa kurejea kwenye matumizi hayo huku mara kadhaa ikiripotiwa kuwa mrembo huyo aliyekimbiza na Kibao cha Na Wewe Milele, amerejea kwenye utumwa huo wa madawa hayo ambayo ni hatari.
Jide alizungumza hayo Ijumaa iliyopita alipokuwa akizindua kichupa chake cha Ndi Ndi Ndi kwenye Kipindi cha Friday Night Live kinachorushwa na East Africa Television na Radio. Alisema alikuwa hajakutana muda mrefu na Ray C kabla ya juzikati alipokwenda kumsalimia nyumbani kwake.
“Ray C alikuja kunisalimia nyumbani, tulizungumza kwa kuwa hatukuwa tumeonana kwa muda mrefu sana, kipindi anachopitia sasa ni kigumu, ni mtu ambaye anahitaji watu wa kuwa naye karibu na marafiki sahihi lakini siwezi kusema kama nilisema namsaidia au chochote.
“Lakini wapo watu ambao aliniambia tayari wapo kwenye mchakato wa kumsaidia, kwa hivyo tunawapa nafasi watu ambao wanaweza kutoa msaada zaidi,” alisema Jide.
Chanzo;GPL