-->

Lissu Kumtetea Wema

Dar es Salaam. Wakati Wakili Tundu Lissu akijitokeza kumtetea msanii maarufu wa fani ya uigizaji wa filamu, Wema Sepetu katika kesi ya kukutwa na bangi, mrembo anayepamba video za wasanii nchini, Agnes Gerald maarufu Masogange (28) amepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kutumia dawa za kulevya.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alijitokeza mahakamani jana kuwa wakili wa Wema na wenzake wawili akiwamo mfanyakazi wa ndani.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Constantine Kakula aliieleza mahakama jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika. Baada ya maelezo hayo, kesi iliahirishwa hadi Machi 15.

Katika tukio jingine, Masogange alipandishwa kizimbani mahakamani hapo akikabiliwa na mashtaka mawili ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroini na oxazepam.

Akimsomea mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbroad Mashauri, Wakili wa Serikali, Constantine Kakula alidai Masogange alitenda makosa hayo kati ya Februari 7 na 14, chini ya kifungu cha 18 (a) cha Sheria ya Kupambana na Dawa za Kulevya namba 5 ya mwaka 2015.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Masogange alikana na Hakimu Mashauri alimtaka mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili; kila mmoja alisaini bondi ya Sh10 milioni na anatakiwa asitoke nje ya Jiji la Dar es Salaam bila kibali cha Mahakama.

Chanzo: Mwananchi

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364