Masogange: Situmii uchawi wanakuja wenyewe
“Wakati nauza sura kipindi kile nilikuwa na akili ya kitoto, yaani nilikuwa nataka na mimi niwe Staa nijulikane. Nilikuwa nikiona wale dada zetu wanavyoonekana kwenye video na mimi nilikuwa natamani vile,lakini sasa hivi najuta kwasababu ustaa nao unanigharimu.
“Sio kwamba wasanii hawanioni hapana wananiona,ila nimeamua kuachana na hiyo kazi, hata boifrendi wangu hapendi kabisa mambo ya kujulikana julikana,yaani mambo ya video queen
hapendi kabisa.
“Nimekua mkubwa na mpenzi wangu hapendi.” Masogange alidaiwa kutumia tunguri kujiongezea mvuto ili kuwanasa vigogo na ikazushwa kwamba etii… kuna waganga wawili wanaompa jeuri mrembo huyo, mmoja akiwa anaishi maeneo ya Mwenge Dar es Salaan na mwingine Bagamoyo Pwani.
“Sijaanza kusikia tuhuma hizo leo lakini mimi si mtu wa mambo ya Kiswahili ujue, nimetoka kwenye familia ya kichungaji, hao vigogo wanakuja wenyewe bila hata ya kutumia ndumba kwani umbo langu tosha ni tunguri,”alisisitiza mrembo huyo.
“Hahahahaa unajua Bongo miyeyusho sana baadhi ya watu na hili umbo langu nimekuwa nikisumbuliwa sana na wanaume lakini kipindi kile niko Sauzi ilikuwa kawaida, ila kiukweli napata tabu hadi naona kero wakati mwingine” alisema Masogange.
Kuhusu madai ya kujihusisha na biashara zisizo halali anasema; “Watu bana!, mimi sina dhiki ya kufikia kuuza mwili wangu eti nipate pesa na kuhusu zile picha kipindi kile nilizopiga hazikuwa za utupu sema basi tu watanzania tunapenda kuzusha sana. Na mtu kuenda Sauzi ndio ameenda kujiuza? Mimi nilikuwa na biashara zangu nafanya na wanaosema hivyo hawanisaidii chochote,hakuna mtanzania anayeninunulia nguo,hayupo anayenipa pesa waongee tu.
“Unajua sisi wadada tuna tabia ya kuoneana wivu akiona unafanya vizuri anaanza kukusemea vitu vya ajabu pembeni,”anasema msanii huyo na kuongeza kwamba amepima ukimwi yuko safi.
Alipeleka Unga Sauzi?
“Unajua watu wengi hawajui hili suala, siku ile (Julai 5, 2013) mimi nilikuwa nasafiri kwenda Sauzi kwa mambo yangu tu, nilipofika pale Uwanja wa Ndege (Julius Nyerere International Airport) nilimkuta huyo mtu ambaye ni Mkongomani ila ameishi sana Tanzania, Yeye tunafahamiana kwa muda mrefu, aliponiona aliniuliza kama na kwenda Sauzi, nikamwambia ndiyo, akasema anaomba nimbebee mizigo yake ya sukari.
“Nilimkatalia, lakini akasema kuna mtu atanipokea Uwanja wa Ndege (wa Kimataifa wa Oliver Tambo) uliopo (Kempton Park)Johannesburg, basi nilimkubalia na nilipoangalia ule mzigo wenyewe kama kweli ni sukari nikaona kweli ni sukari tena ile nyeupe, nilimwambia kama anataka nimsaidie kuufikisha Afrika Kusini.
“Apeleke mpaka kwenye ndege ili kunipunguzia kazi ya kubebabeba, nikifika Sauzi nitamtolea huyo mtu sukari yake, akapeleka mpaka kwenye ndege, mimi nikapanda na safari ikaanza.”
“Tulifika uwanja wa ndege salama,nikashuka na yale mabegi , lakini cha ajabu wakatokea askari na kutukamata huku wakiniuliza nimebeba nini? Nikawaambia sukari, wakasema siyo sukari, wakanitaka nilambe, kulamba hivi, ndiyo nikajua kweli siyo sukari, tukawekwa chini ya ulinzi na kupelekwa kwenye vyombo vyao vya sheria kwa hatua zaidi.
“Yaani Sikuwa namjua kwa sura huyo mtu ambaye niliambiwa atapokea huo mzigo ,ila nilipewa mawasiliano yake tu kuna uwezekano alituona wakati tumekamatwa na polisi maana tulizungukwa na watu wengi.”
Masogange na mwezake, Melisa walikamatwa Julai 5, mwaka jana kwenye uwanja huo wa ndege nchini humo wakiwa na madawa hayo yaliyokadiriwa kuwa na thamani ya shilingi bilioni 6.8.
Kesi yake iliendeshwa na Mahakama Kuu ya Gauteng iliyopo Kempton Park nchini humo na alikutwa na hatia ambapo alihukumiwa kwenda jela miezi 32 au kulipa faini ya randi 30,000 (Sh4.8milioni). Masogange alilipa faini huku mwenzake, Melisa akiachiwa huru kukutwa hana hatia.
Masogange alizaliwa Aprili 23,1988 kwenye hospitali ya mkoa wa Mbeya. Shule ya msingi na sekondari alisoma pale Sangu ndio baadae akaibuka zake Dar kusaka mahela.
By RHOBI CHACHA, Mwanaspoti