-->

Mwasiti: Wanawake Tuwekeze Kwenye Ardhi Siyo Nywele

MSANII wa muziki wa Zouk, Mwasiti Almasi, amewaasa wanawake waachane na matumizi mabaya ya fedha kwa kununua nywele, vipodozi na nguo za gharama, badala yake watumie fedha hizo kuwekeza katika ardhi.

Mwasiti

Mwasiti anawaasa wanawake wenzake kuelekea maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani inayoadhimishwa kesho ambapo msanii huyo na wenzake watatu watatumbuiza katika tamasha maalumu litakalofanyika mkoani Mtwara.

Mkali huyo wa wimbo wa ‘Sema Nae’, alisema umefika wakati mabinti kuamka na kuona thamani yao kwa kuandaa maisha yao ya baadaye badala ya kuwategemea wanaume kwa kila kitu.

Alisema ikiwa mabinti wataelimika kwa kuanza kuwekeza katika ardhi na vitega uchumi mbalimbali, itakuwa ni nafasi nzuri ya kujiepusha na unyanyasaji wa kijinsia, kuliko kununua vito vya gharama kubwa.

Pia Mwasiti aliwataka wananchi wa mkoa huo wa Mtwara wajitokeze kwa wingi katika maadhimisho hayo, kwa kuwa pia shindano linaloendeshwa na Shirika la Kimataifa la Oxfam Tanzania la Mama Shujaa wa Chakula kwa mwaka 2016 litazinduliwa.

Kwa upande wa msanii wa nyimbo za asili, Vitali Maemba, anasema anachukizwa na tabia ya baadhi ya wanaume wanaowabeza wanawake wakati ni nguzo ya familia katika malezi ya watoto, usalama wa familia na pia wanahakikisha usalama wa chakula unapatikana.

Naye mwanamuziki wa muziki wa dansi nchini, King Dodo la Buche, alisema ufanikishaji wa uzinduzi huo utaleta changamoto chanya kwa wazawa na kulifanya Taifa kupiga hatua zaidi kimaendeleo.

Oxfam imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Serikali kupitia Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi, pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi kupitia mradi wa Mama Shujaa wa Chakula na pia kufanya kazi mbalimbali, ikiwemo ugawaji hati miliki za kimila katika vijiji vya mikoa ya Morogoro na Simiyu.

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364