-->

Mwigulu: Aliyemtishia Nape Bastola si Polisi

Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amesema mtu aliyemtishia kwa bastola aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye si askari wa Jeshi la Polisi, lakini ameshapatikana na atashughulikiwa kwa mujibu wa utaratibu wa ulinzi na usalama.

Mtu Aliyemtishia Nape

Mwigulu alisema hayo baada ya kufungua mkutano wa kazi wa mwaka wa maofisa waandamizi wa polisi, makamanda wa mikoa na wakuu wa vikosi wa Jeshi la Polisi ambao unafanyika mjini hapa.

“Ameshapatikana (aliyemtishia Nape) na atashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za ulinzi na usalama ambazo zimekuwa zikifanyika ndani, lakini hazitangazwi,”alisema.

Hata hivyo, Mwigulu alikataa kuelezea kwa undani kuhusu mtu huyo kwa kubainisha anatoka taasisi gani wala jina la mtuhumiwa kwa madai kuwa ni kwa sababu ya usalama wake.

Baadhi ya taasisi za ulinzi na usalama nchini ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Usalama wa Taifa na Takukuru.

Mtu huyo alifanya kitendo hicho wakati Nape, ambaye alikuwa Waziri wa Habari, alipokuwa anaelekea Hoteli ya Protea alikopanga kuzungumza na waandishi wa habari baada ya mbunge huyo wa Mtama kuachwa katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri.

Mtu huyo alikuwa pamoja na wenzake wawili ambao kwa pamoja walikuwa wakimlazimisha arudi kwenye gari lake na kuondoka, lakini Nape alibisha na ndipo mtu huyo aliporudi nyuma, kuchomoa bastola kutoka kiunoni na kisha kumtishia kabla ya kutulizwa na mwenzake.

Watu hao walitoweka eneo hilo muda mfupi baadaye.

Siku moja baada ya tukio hilo Mwigulu alimwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi, Ernest Mangu kumtafuta mtu huyo.

Mwigulu aliandika katika ukurasa wake wa twitter akisema:

“Mh Nape sio jambazi, hana record za uhalifu. Kitendo cha kutolewa bastola si cha Kitanzania na si cha kiaskari. Nimemuagiza IGP achukue hatua.”

Tukio hilo lilitokea siku chache baada ya kiongozi mmoja kuvamia kituo cha televisheni cha kampuni ya Clouds Media, akiwa na askari wenye silaha za moto na kulazimisha arekodiwe mahojiano baina ya watangazaji wa kipindi cha Shirika la Wambeya Duniani (Shilawadu) na mwanamke anayedai kuzaa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ambaye ameibukia kuwa mpinzani wa kiongozi huyo.

Hadi sasa, Jeshi la Polisi halijaeleza kuhusu askari hao waliojumuika kufanikisha uvamizi huo.

Tukio la Nape kutishiwa bastole limelaaniwa na watu mbalimbali.

Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu aliahidi kulifikisha suala hilo bungeni.

Awali wakati akifungua mkutano huo jana, Mwigulu aliwataka maofisa hao kutafuta utaratibu mwingine wa kuwakamata madereva wa bodaboda badala ya kuwafukuza kwa sababu imekuwa ni miongoni mwa vyanzo vya ajali za barabarani.

Pia Mwigulu amepiga marufuku tabia ya polisi kuwabambikizia ama kuwabadilishia kesi watuhumiwa akisema baadhi yao wamekuwa wakiomba rushwa kwa watuhumiwa ili waweze kutekeleza hayo.

Alisema tatizo la vifo na ajali zinazotokana na vyombo vya moto kama pikipiki, ni kubwa nchini.

Alisema ajali 7,000 zilizohusisha pikipiki zilitokea mwaka jana wakati idadi ya vifo vinavyotokana na ajali ilikuwa 2,000. Alitaka jambo hilo liangaliwe kwa jicho la pekee kwa kutafuta mbinu mpya za ukamataji.

“Hivi sasa mbinu zinazotumiwa na askari zimekuwa zikiwatia hofu madereva na kujikuta wakiishi kama digidigi. Hata pale wanapokuwa hawana kosa, wanakimbia na matokeo yake wanasababisha ajali,” alisema.

Aliwasihi kutofautisha madereva wa pikipiki wenye makosa, ambao alisema wanatakiwa kufikishwa kituoni, na wasio na makosa ambao wanatakiwa kuachiwa.

Kuhusu kubambikizwa makosa, Mwigulu alisema vitendo hivyo ni kinyume cha sheria.

Alisema pia baadhi yao wamekuwa wakiwabadilishia kesi watuhumiwa kinyume cha maadili ya Jeshi hilo.

Mwigulu alisema jambo hilo linatokana na baadhi ya askari hao kunyimwa rushwa wanapoomba na kuamua kutumia madaraka yao vibaya.

Naye mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Adadi Rajabu aliwataka makamanda hao kuwashauri wakuu wa mikoa kuhusu sheria na utaratibu badala ya kungoja hadi mambo yanaharibika ndipo wawaambie.

“Ni vyema mkawashauri wanapokwenda kinyume cha sheria na taratibu si kusubiri mambo yaharibike ndipo mshauri,” alisema.

Kwa upande wake, aliyekuwa Waziri Mkuu, John Malecela alisema baada ya uhuru, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alisema hawezi kuwanyeshea pesa kama mvua hivyo umasikini utaendelea kuwepo.

Alisema Mwalimu aliwahakikishia kuwa baada ya kupata uhuru jambo watakalolipata ni heshima.

“Hivyo mkiwapa heshima wananchi mnaowalinda na mali zao, mtakuwa mnatekeleza maagizo ya Mwalimu Nyerere,” alisema.

Awali IGP Mangu alisema mkutano huo wa siku tatu unabeba kauli mbiu ya “Zingatia Maadili Tunapopambana na Uhalifu ili Kuimarisha Usalama kwa Maendeleo ya Taifa” ambao unamtaka askari kufanya kazi kwa weledi, utu na usawa.

Chanzo:Mwananchi

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364