-->

Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe Afungukia Ishu ya Mzee Majuto Kudhulumiwa Mamilioni

Waziri wa Habari,  Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amefunguka na kusema kuwa Mzee Majuto amedhurumiwa pesa milioni 25 na kampuni ya filamu ambayo jina lake amelihifadhi na kudai atatumia hata mshahara wake kuhakikisha anawafunga watu hao.

Mwakyembe amesema hayo leo Oktoba 27, 2017 alipokutana na wasanii mbalimbali kujadili changamoto za kazi ya sanaa nchini na kusema katika vitu ambavyo atapambana navyo ni pamoja na watu wanaowadhurumu wasanii haki yao na kuwaibia kazi zao za sanaa.

“Nilipopita Tanga nilikutana msanii nguli wa filamu Mzee Majuto nilikwenda kumjulia hali na bahati nzuri saizi anaendelea vizuri, Mzee Majuto akaniomba kitu kimoja na kuniambia naumwa nahitaji pesa lakini nimeshafanya kazi na kampuni hii akanionyesha na kuwa ameshatengeneza filamu zaidi ya 100 na kampuni hiyo kwa mkataba wa kulipwa fedha ndogo tu shilingi milioni 25 lakini huu ni mwaka wa  pili hajalipwa hata senti tano sasa hayo ndiyo mambo ambayo sifurahii, nimeshapeleka taarifa kwa hiyo kampuni tukutane Dar es Salaam na Dodoma asipokuja tunajua njia za kumsafirisha kwenye kalandinga mpaka Dodoma, huu ni wizi kama wizi wa kwenda kumchomolea mtu mfukoni” alisisitiza Mwakyembe

Waziri Mwakyembe aliendelea kufafanua kuwa kwa sasa yupo tayari kutumia pesa zake mfukoni kuhakikisha Mzee Majuto anapata haki yake kwa kazi mbalimbali alizofanya na kampuni hiyo.

“Mzee Majuto alikwenda Mwanza na familia kupokea ule mzigo, meneja kwa kumuheshimu akamfuata na kumwambia hiyo cheki hata senti tano hakuna na cheki iliyobaundi ni kosa la jinai, tunachezea watu hivi. Mzee Majuto ameacha familia yake, amekaa Mwanza zaidi ya miezi sita anahangaika kuzipata hizo pesa, na mimi niko tayari nitatumia hata mshahara wangu twende mahakamani tufunge watu tumeshachoka huko ni kudharau watu” alisema Mwakyembe

Mwezi Agosti Waziri Mwakyembe alimtembelea msanii nguli na mkongwe wa filamu nchini Mzee Majuto nyumbani kwake ambapo alikwenda kumjulia hali baada ya kupata taarifa kuwa anaumwa.


EATV.TV

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364