Nape Kutumbua Majibu 4 Ambayo Yataibadili Bongo Movie
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametaja mambo manne ambayo ni vikwazo ndani ya sekta ya sanaa ya filamu nchini na kuyaita kwamba ni majipu huku akisisitiza kwamba Serikali itatunga sera ya sekta hiyo katika mwaka wa fedha 2016/17.
Nape aliyataja mambo hayo na kuyafananisha na majipu kuwa ni uporaji wa kazi za wasanii nchini, ujenzi duni wa miundombinu ya kazi za wasanii, usimamizi mbovu wa Bodi ya Filamu, sanjari na tatizo la mfumo mbovu wa usambazaji wa kazi za wasanii.
Akizungumza wakati akizindua tamasha la filamu la Tanzanite International Film Festival (TIFF) jijini Arusha juzi ambalo lilihudhuriwa na wasanii maarufu wa filamu nchini, waziri huyo alisema kwamba jipu la kwanza ambalo atakwenda kulitumbua ni uporaji wa kazi za wasanii nchini.
Hata hivyo, alisema kwamba jipu la pili ni ujenzi duni wa miundombinu ya kazi za wasanii za filamu na kudai kwamba chini ya uongozi wake atahakikisha anaimarisha miundombinu bora kwa lengo la kuwasaidia wasanii hao pamoja na kulinda haki zao.
Alisema ya kwamba mfumo wa kazi za usambazaji wa kazi za wasanii nchini pamoja na hakimiliki ni wa kinyonyaji huku akitolea mfano wa kazi za msanii maarufu wa sanaa hiyo nchini, Steven Kanumba na kusema kwamba familia yake hainufaiki na matunda ya kazi zake hadi sasa kutokana na mfumo mbovu wa usimamizi wa kazi za wasanii. Alitaja takwimu kwamba mwaka 2011/12, filamu 218 zilitengenezwa nchini na mwaka 2014/15 kazi hizo ziliongezeka hadi kufikia 1,400.
Source:Mwananchi