Ndugai Abariki Kutimuliwa Wabunge Nane CUF
Spika wa Bunge, Job Ndugai, ameikubali barua aliyoandikiwa na Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekti wa CUF anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, kuwatimua uanachama wabunge wake wanane wa viti maalum.
Hatua hiyo ya Spika Ndugai inamaanisha kuwa wabunge hao wamepoteza viti vyao Bungeni na chama hichi kitatakiwa kuwateua wanachama wengine kuziba nafasi hizo.
Taarifa iliyotolewa na Bunge jioni hii inasema Spika amechukua uamuzi huo kwa mujibu wa ibara ya 67(1)(b).
Spika ametoa uamuzi huo siku moja tu baada ya kueleza kupokea barua ya Profesa Lipumba na kusema anaitafakari kabla ya kutoa uamuzi wake.
Taarifa ya Bunge imewataja wabunge waliopoteza nafasi zao kuwa ni Severina Mwijage, Saumu Heri Sakala, Salma Mwassa na Riziki Mngwali.
Wengine ni Raisa Mussa, Miza Bakari Haji, Hadija Al-Qassmy na Halima Mohammed.
Profesa Lipumba alisema wiki iliyopita kuwa wanachama hao wamefukuzwa kutokana na utovu wa nidhamu na kukiuka katiba ya chama.
Alisema wabunge hao waliitwa ili kujitetea lakini wakakaidi na hivyo Baraza Kuu la Uongozi halikuwa na uamuzi mwingine zaidi ya kuwafukuza uanachama.
Pamoja nao, wabunge wengine wawili nao waliitwa lakini wamesalimika kwa sababu waliitaarifu kamati hiyo kuwa wamebanwa na majukumu mengine.
Aidha, Profesa Lipumba alisema timuatimua hiyo itaendelea ikimhusisha pia Katibu Mkuu wa chama hicho, Seif Sharif Hamad, ambaye hajafika makao makuu ya chama hicho kwa kipindi kirefu.