Rais Magufuli Asema Epa ni Ukoloni Mwingine
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemweleza Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kwamba Mkataba wa Ushirikiano wa Uchumi na Jumuiya ya Ulaya (EPA) ni aina mpya ya ukoloni utakaoua maendeleo ya viwanda katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Siku ya mwisho ya kusaini mkataba huo ilikuwa Oktoba mosi mwaka jana, lakini katika kikao cha wakuu wa EAC kilichofanyika jijini Dar es Salaam Septemba, Uganda na Tanzania ziliomba muda uongezwe kwa miezi mitatu zaidi ili waliangalie suala hilo kwa makini zaidi.
Tayari, Kenya na Rwanda zimeshasaini mkataba huo katika hafla iliyofanyika makao makuu ya EU yaliyoko Ubelgiji.
Rais Magufuli alisema hayo jana Ikulu, jijini Dar es Salaam baada ya mazungumzo na Rais Museveni ambaye yupo nchini kwa ziara rasmi ya siku mbili baada ya kualikwa na mwenyeji wake wakati walipokutana Addis Ababa, Ethiopia katika mkutano wa Umoja wa Afrika (AU).
Mazungumzo hayo yaliambatana na utiaji saini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Uganda uliosainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Dk Augusine Mahiga na mwenzake wa Uganda, Oryem Henry Okello.
Akizungumza na vyombo vya habari, Magufuli alisema amempa Museveni timu ya wataalamu wazuri ili walifafanue suala hilo kwa undani zaidi na Machi 18 mwaka huu, timu hiyo itakwenda Uganda kwa kazi hiyo. Mazungumzo ya wakuu wa nchi za EAC yaliyofanyika Dar es Salaam Oktoba, mwaka jana hayakufikia mwafaka, jambo lililowalazimu viongozi hao kujipa muda wa miezi mitatu zaidi kwa ajili ya kulijadili suala hilo.
“Wataalamu wetu watakwenda Uganda kutoa maelezo zaidi kuhusu suala hili. Huwezi kupanga kuendeleza viwanda vyako wakati umesaini mkataba utakaokukwamisha,” alisema Rais Magufuli.
Katika kutafuta kuungwa mkono msimamo huo wa Tanzania, Rais Magufuli alisema: “Museveni alibebwa sana wakati wa (Rais Julius)Nyerere. Kwa kuwa Nyerere hayupo basi naye anibebe mimi kwa kufanya haya ninayoyataka.”
Kiongozi huyo alisisitiza kwamba Watanzania na Waganda ni ndugu kwa sababu walimwaga damu wakati wa vita wakipigana kumuondoa kiongozi wa kijeshi, Idd Amin. Alisema undugu huo una historia ndefu na kwamba wataendeleza umoja huo kama ilivyokuwa zamani.
Kwa upande wake, Rais Museveni alisema jambo la Epa linahitaji msimamo wa pamoja, jambo ambalo alisema limekuwa gumu kwa viongozi wengi wa Afrika. Alisema suala hilo lazima lizungumzwe kwa kina ili nchi za Afrika Mashariki zinufaike. “Jambo dogo namna hii tunakosa msimamo, sasa tutaweza nini? Uhusiano wetu ni jambo muhimu zaidi kuliko hao Europeans (wazungu),” alisema Rais Museveni na kushangiliwa zaidi na upande walikokaa viongozi wa Tanzania.”
Miradi ya maendeleo
Rais Magufuli, ambaye pia ni mwenyekiti wa EAC, amemweleza Museveni kwamba Serikali ya Tanzania itajenga bandari kavu mkoani Mwanza ambayo itakuwa maalumu kwa mizigo inayotoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Uganda pekee. Alisema ujenzi wa bandari hiyo utaenda sambamba na ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge) itakayotoka Dar es Salaam mpaka Mwanza – Isaka. Aliongeza kwamba Serikali yake imekarabati kivuko cha MV Umoja kitakachosaidia kusafirisha mizigo.
Viongozi hao walijadili pia kukuza biashara kati yao na kuongeza uwekezaji. Alisema mwaka jana biashara kati ya Tanzania na Uganda ilikuwa na thamani ya Sh178 bilioni, lakini mwaka huu imefikia Sh193.5 bilioni.
Uwekezaji wa Uganda nchini umefikia dola 146 milioni za Kimarekani. Hata hivyo, Rais Magufuli alisema kiwango hicho bado kiko chini, hivyo wanahitaji kuongeza kasi zaidi ya biashara ili kukuza uchumi wao.
Rais Museveni alimpongeza Rais Magufuli na kusema anafuata nyayo za Mwalimu Julius Nyerere katika utendaji wake. Kiongozi huyo amelikaribisha Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) kufanya safari zake nchini humo.
Chanzo:Mwanachi