Sakata la Filamu za Nje: Makonda Amueleza Haya Rais Magufuli
Jumamosi hii Rais John Pombe Magufuli alikuwa katika uzinduzi wa mabweni ya Chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM) ambapo Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda alipata fursa ya kuzungumzia mambo mbalimbali yanayoendelea ndani ya mkoa wake na kuzungumzia ishu ya operesheni yake mpya ya kupiga vita filamu za nje ambazo hazilipi kodi.
Filamu hizo zinadaiwa kuinyima serikali mapato pamoja kubana vipato vya wasanii wa ndani kwa kuwa wananchi hununua filamu hizo kwa bei ya chini na kuacha za wasanii wa ndani ambazo zina bei ya juu.
Akiongea katika halfa hiyo, RC Makonda amesema biashara hiyo imeweza kusababisha maduka mengi ya filamu za ndani kufungwa kutokana na wateja wengi kuhamiwa kwenye maduka ya filamu za nje ambayo uuzwa filamu kwa bei ya chini.
“Mh Rais wasanii unaowaona leo hapa wanachangamoto moja kubwa sana ambayo nichukue fursa hii kumpongeza Waziri wa Habari na Utamadani Dr. Harrison George Mwakyembe, tumeshirikiana naye vizuri. Zipo CD mtaani zinauzwa kwa bei ya chini kabisa jambo ambalo linaua soko la wasanii wetu wa ndani na mwisho wa siku wanabaki kuwa ombaomba, ukimuangalia JB, Ray Kigoni na wasanii wengine ambao wamekuja hapa wamekosa matumaini kuhusu maisha yao,” alisema RC Makonda.
“Mh Rais sisi wasaidizi wako, tumeamua kuitafsiri ndoto yako yakuwapigania na kuwatetea wanyonge. Kariakoo kulikuwa na maduka 300 ya kuuza filamu za wasanii wa ndani lakini sasa hivi yamebaki mawili tu. Maduka mengi yaliyobaki Kariakoo ni maduka ambayo yana-download filamu kwenye mitandao na kuzizalisha pamoja na kuzisambaza mtaani na wanaziuza kwa bei ya chini wakati ukienda Nigeria hawaruhusiwi kuuza filamu za nje,”
“Ukienda Ghana hauruhusiwi kuuza movie za nje ya Ghana. Wasanii wetu wanapeleka laki tano bodi ya filamu, wanapeleka laki tatu kwajili ya kupewa kibali, wanapeleka elfu moja kila dakika moja pale filamu zao zinapokwenda kukaguliwa na Bodi ya Filamu ili iweze kupitishwa na kuonekana inafaa kuonekana ndani ya rika fulani, wanalipa kodi ya asilimia 30 ya mapato yao. Lakini wale wanaoingiza filamu kutoka nje hawalipi kodi, yaani hawalipi chochote kwa sababu ni kazi za wizi ambazo zimekuja kuikandamiza tasnia ya filani. Sisi kama vijana wako tumeamua kuifanya hii kazi na wiki ijayo tunaanza oparesheni. Kwahiyo Mh Rais ukisikia kuna kelele huko wanaolia ni wengi, wacha na sisi tuendelee kuwaliza ili wanyonge wapate haki zao,” aliongeza.
Alisema ndani ya Kariakoo kuna duka moja lina mzigo wa zaidi ya tsh bilioni 4 lakini hawalipi kodi hata mia.
Bongo5