Serikali Iruhusu Bangi – Afande Sele
Msani mkongwe wa Hip Hop ambaye alitupa karata yake kwenye siasa na kufeli Afande Sele, ameitaka serikali kuruhusu biashara na matumizi ya bangi, ili kuongeza pato la taifa kwa kuilipia kodi biashara hiyo.
Akiongea kwenye kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa Radio, Afande Sele amesema iwapo zao hilo la biashara likiruhusiwa rasmi nchini na kuwekewa mfumo maalum wa matumizi itasaidia kukuza uchumi.
“Hatuna barabara, hatuna madawa hospitalini, hatupati fedha kwa sababu hatupati fedha nyingi kwenye kodi zetu, lakini tungeingiza bangi kwenye mfumo wenye kuruhusiwa na tukaweza kuiwekea mazingira rasmi ya matumizi yake tukauza ndani na nje ya nchi tungeweza kukusanya kodi kwa kiasi kikubwa sana, tungejenga nchi yetu”, alisema Afande Sele.
Pamoja na hayo Afande Sele ameonyesha kushangazwa na kitendo cha serikali kukataza bidhaa hiyo ambayo inajumuishwa kwenye madawa ya kulevya, na kuingiza rizla ambazo hutumika kusokotea bangi.
“Taifa tupige hatua lazima tuachane na vitu flan vyenye unafiki, Tanzania wengi wanasema sivuti bhangi lakini upande wa pili wanavuta, au serikali inasema ina sheria za kuzuia bangi lakini bangi zinalimwa vijijini huko bangi zinauzwa na serikali hii hii ambayo ndio inaingiza rizla bandarini zinalipiwa kodi, lakini zile rizla hazina kazi yoyote katika taifa kama sio kunyongea bangi kwa hiyo serikali inafahamu na viongozi wanafahamu lakini bahati mbaya kuna unafiki”, alisema Afande Sele.
EATV.TV