-->

Zari, Diamond Kimenuka Ulaya!

Diamond-Platnumz-8Mbongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ akiwa Sweeden na familia yake.

DAR ES SALAAM: Hakuna furaha isiyo na karaha! Ndiyo kauli inayoweza kutumika kwenye habari ya ziara ya Mbongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Familia ya Wasafi Classic Baby (WCB) huko barani Ulaya ambapo staa huyo na mama mtoto wake, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, wanadaiwa kukinukisha, kisa kikidaiwa ni wivu wa mapenzi, Amani limenyetishwa.

NI MUDA MFUPI BAADA YA KUTUA SWEDEN
Habari kutoka kwa chanzo chetu makini ambacho ni mmoja wa watu waliopo kwenye msafara wa ziara hiyo iliyopewa jina la From Tandale to the World, zilidai kuwa, mwishoni mwa wiki iliyopita, Zari na Diamond walitibuana muda mfupi baada ya kutua katika Jiji la Stockholm nchini Sweden kwa ajili ya shoo.
Kilidai kwamba, Diamond alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuvamiwa na warembo wakimtaka kimapenzi huku Zari akishuhudia.

CHANZO CHATIRIRIKA
“Huku kuna ishu ambayo ni nyeti sana maana kilichomkuta Diamond kwa Zari walipofika hotelini kama isingekuwa sisi kuokoa jahazi basi hata shoo zingeharibika maana wivu wa Zari uliharibu hali ya hewa kiasi cha kujikuta mama Diamond (Sanura Kassim a.k.a Sandra) akibaki njia panda na kujuta kusafiri.

MAMA D AFANYA KAZI YA ZIADA
“Ilibidi mama Diamond kufanya kazi ya ziada ya kusuluhisha ugomvi ambao ulitokana na vimwana wa Kibongo waishio huku (Sweden), kumvamia Simba (Diamond) wakiashiria kumtaka kimapenzi huku Zari akishuhudia laivu.

“Unaambiwa mambo yaliharibika hatari, kila mmoja akalala kwenye chumba chake. Sema Diamond ana moyo wa kiume tu la sivyo angekuwa naye ni mtu wa kususa basi Salam (mmoja wa mameneja wa Diamond) na mama Diamond wangepata shida zaidi kwani Zari hakuna somo alilokuwa akielewa hata kidogo juu ya msala huu.

“Huwezi kuamini baada ya kumuona Diamond amegandwa na warembo, Zari akajua ni mademu zake labda alijuana nao siku nyingi.

“Ishu ilikuwa hivi; siku hiyo baada ya kufika hotelini na mashabiki wa Sweden kujua kuwa tayari timu nzima ya Wasafi ipo hapa, tulishangaa kuona watu wakija hotelini kumuulizia Diamond, jambo ambalo hata sisi lilitushangaza kwamba walijuaje kama yupo ndani ya nyumba?

“Ukiacha hilo, tulishangaa zaidi wakati tunajiandaa kwenda kuuona ukumbi wa kufanyia shoo yaani wakati wa ‘rehearsal’ kulifumka umati ukitaka kupiga picha na sisi na baadaye ndiyo watu wakatutokea hadi hotelini,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:

“Hata hivyo, utu uzima dawa kwa sababu mama Diamond na Salam walifanikiwa kuwaweka sawa na hata ukumbini walikwenda pamoja japokuwa Zari alionekana kutii wito kwa shingo upande kama anavyosema Harmonize kwenye wimbo wake wa Aiyola.”

HUYU HAPA DIAMOND
Baada ya kupenyezewa ‘ubuyu’ huo, Amani lilifanya juhudi za hali na mali ili kupata majibu kutoka kwa Diamond kama ni kweli ‘mtiti’ huo ulimkumba kiasi cha kumfanya atofautiane na mama Tiffah ambapo alipopatikana kwa njia ya WhatsApp alifunguka ‘eituzedi’.

Diamond alisema suala la msanii kutoka nje ya nchi na kujikuta akipapatikiwa na watu ni jambo la kawaida kwani mapenzi ya mashabiki wa ndani na nje ya nchi huwa ni tofauti hivyo kama ukiwa na mke au mpenzi wako na ukawa hujamjulisha hilo lazima mtajikuta mkizinguana.

AKIRI KUTOFAUTIANA
“Kusema kweli mimi nilipokelewa vizuri karibia kila sehemu nilipoanzia kufanya shoo zangu na hapa Sweden kweli watu wameonesha hamasa kubwa kupita kiasi, ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba suala la mimi na mama mtoto wangu kutofautiana si vyema kuliweka wazi ila ikumbukwe tu kuwa kutofautiana kwa wapenzi mnapokuwa pamoja hilo lipo tu maana binadamu tumeumbwa hivyo.

“Ninachoweza kusema kwa sasa mimi na Zari tuko poa, mambo yanaenda vizuri na ndiyo maana utaona hata siku hiyo kabla ya kuingia ukumbini alikuwa karibu sana na mimi na ilibidi niingie naye ili kila mtu ajue kama niko na mama mtoto wangu kwani bila kufanya hivyo kuna warembo wenye asili ya Kiafrika wakikuona kama hawajui kweli inakuwa rahisi kukuibukia hata mbele ya mke wako.

“Pia ifahamike tu kuwa mimi ni msanii hivyo mashabiki wangu ni wa aina zote, huwezi kuwabagua wala kuwatofautisha hivyo namshukuru mama Tiffah amelijua hilo na sitarajii kama anaweza kukwazika tena na shabiki kunivaa au kuniambia lolote maana si kila shabiki anajua kama nimesafiri na familia,” alisema Diamond.

ZIARA INAENDELEA
Kabla ya kutua Sweden, Diamond na Wasafi walianzia Ujerumani kisha kufunika kwa shoo kali na sasa ni zamu ya Ubelgiji na nchi nyingine barani Ulaya.

Waandishi: Musa Mateja

GPL

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364