-->

Simu Yamponza Aliyejitosa Baharini

Zanzibar. Msichana aliyejirusha baharini juzi, alikimbia kwao Zanzibar baada ya kukutwa na simu kinyume na utamaduni wa familia yao.

Msichana huyo, ambaye jina tunalihifadhi kwa sababu za kimaadili kutokana na kuwa na umri mdogo, alikuwa amepanda boti ya Kilimanjaro iliyokuwa ikisafiri kwenda Zanzibar juzi na alijirusha katika Bahari ya Hindi saa 5:15 asubuhi.

Picha za video zilizosambaa mitandaoni zinamuonyesha msichana huyo akiwa amelala chali baharini huku mikono akiwa ameinyoosha pembeni kumwezesha kuelea, wakati mabaharia wa boti hiyo wakijongea kwenda kumuokoa.

Mama mdogo wa msichana huyo na ambaye ndiye mlezi wake, Asha Saleh Manzi aliliambia gazeti hili nyumbani kwao Kikwajuni jana kuwa msichana huyo mwenye umri wa miaka 16, ni mwanafunzi wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari ya Glorious iliyopo kisiwani Unguja.

Alisema hajui sababu hasa iliyomfanya binti huyo kukimbilia Dar es Salaam Alhamisi iliyopita na baadaye kujitosa baharini.

Hata hivyo, Manzi anayeishi na binti huyo ambaye mama yake mzazi yupo Muscat, Oman alisema Jumatano alibaini kuwa alikuwa na simu ya mkononi kinyume na masharti waliyompa.

Alisema familia ilimtaka kuitoa simu hiyo, ikimtisha kwamba asipofanya hivyo angefikishwa kituo cha polisi ili achukuliwe hatua za kisheria.

Manzi alisema baada ya kutishwa alieleza kuwa simu ipo kwa shoga yake ambaye aliwapa walipomfuata.

“Tulirudi nyumbani. Tulimwambia asubuhi ni lazima atuambie simu ameipata wapi, la sivyo tutachukua hatua zaidi dhidi yake ikiwa ni pamoja na kumfikisha polisi. Wakati huo simu tulimwachia,” alisema Manzi.

Walipokwenda chumbani kwake asubuhi, hawakumkuta na ndipo walipoanza kuwasiliana na ndugu na jamaa kujua alipo, wakiwamo wanaoishi Dar es Salaam.

Manzi alisema waliwasiliana na rafiki zake, akiwemo mmoja wa kiume ambaye aliwaeleza kuwa alikuwa akiwasiliana naye.

“Katika mawasiliano hayo, alisema yupo kwa dereva wa teksi ambaye alimuokota bandarini Dar es Salaam akiwa anahangaika,” alisema Manzi.

Alisema waliwasiliana na ndugu zao waliopo Dar es Salaam ambao baada ya kuwasiliana na mtu aliyedai alimuokota walimkuta na kumchukua.

“Alifika Dar Alhamisi, lakini ndugu zetu walimpata Ijumaa. Alilala kwa huyo dereva wa teksi siku moja. Uamuzi ulifikiwa kwamba arudishwe Zanzibar na ndipo Jumatatu aliondoka na mjomba wake, ambaye wakati wa tukio hilo (la kujitosa baharini) alikuwa naye pembeni,” alisema.

Kauli ya mjomba

Akizungumzia mkasa huo, Mgeni Abrahman Mgeni, mjomba wa binti huyo aliyesafiri naye kwenye boti kutoka Dar es Salaam, alisema waliondoka vizuri nyumbani kwao hadi walipoingia kwenye boti.

Alisema walipokaribia Chumbe, msichana huyo alimwambia hajisikii vizuri na kumuomba wahamie eneo la nje ili apate hewa safi.

Mgeni alisema hakumkatalia ombi lake kwa kuwa hali ya bahari haikuwa nzuri siku hiyo. Alisema walitoka hadi kwenye varanda ya boti na wote wawili walikaa sehemu moja.

Alisema dakika chache baadaye, binti huyo alimwambia ampatie kitambaa chake cha kujifunika usoni na baibui akidai muda wa kufika Zanzibar unakaribia, hivyo anataka avae ili kuondoa usumbufu wakati wa kushuka.

Mgeni alisema alikubaliana na ombi hilo na alipogeuka upande lilipokuwa begi, ndipo ghafla msichana huyo alipojitosa baharini na kuanza kupiga yowe.

“Niliangalia kumbe ni yeye (anamtaja jina). Tulishirikiana na mabaharia wa boti hiyo ili kumwokoa, kitendo ambacho kilifanikiwa kwa dakika chache tu,” alisema.

Mgeni aliyezungumza na gazeti hili jana saa 4:00 asubuhi alisema hajui ni nini hasa kilichomfanya mjomba wake achukue uamuzi wa kujitosa baharini.

Tabia ya msichana huyo

Mama yake mdogo, Manzi alisema tangu msichana huyo akiwa mdogo, amekuwa na tabia nzuri.

Alisema ni mtoto ambaye hana mashoga wengi na si mtu wa kujiingiza katika makundi maovu na mara nyingi hushinda ndani.

Alisema wengi wanaofika nyumbani kwao hushangaa kumuona anashinda ndani tu, hata wakati mwingine humwambia atoke angalau nje, lakini hapendi.

Manzi alisema takriban miezi miwili walianza kupata taarifa za mabadiliko ya tabia yake shuleni.

“Tulipigiwa simu na mwalimu wake akitutaka tufike shuleni. Tuliitikia wito huo. Mwalimu alituambia mbona (anamtaja jina) ameanza kubadilika,” alisema.

Manzi alisema walimu waliwaeleza kuwa msichana huyo ameanza kuonekana akitumia simu na kwamba amechangamka tofauti na alivyokuwa awali.

“Hatukubishana na mwalimu tukamwambia tuachie hili tutalifanyia kazi,” alisema.

Kuhusu hali ya msichana huyo, Manzi alisema inaendelea vizuri na kwamba wameshauriwa na daktari wasizungumze naye kuhusu tukio hilo.

“Juzi baada ya kurudi nyumbani kutoka kwa daktari huko Kidongo Chekundu tulipewa dawa ili tumpatie. Tunashukuru tulipompa, alipata nguvu za kula ila hatujazungumza jambo jingine. Tumefanya hivyo ili kufuata maagizo ya daktari,” alisema.

Kamishna Msaidizi wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Hassan Nassir Ali alisema bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kujua chanzo.

Alisema ikibainika kuwa msichana huyo alijitosa bahari kwa lengo la kutaka kujiua, atafikishwa mahakamani.

Hiyari Miraji Othman (58) na ambaye anafanya kazi nyumbani kwa binti huyo, alisema msichana huyo hana tabia mbaya wala hakumbuki tukio lolote la ajabu alilowahi kufanya.

Alisema kwa zaidi ya miaka kumi sasa yupo ndani ya nyumba hiyo akifanya kazi na anamtambua kuwa ni miongoni mwa watoto waliolelewa vyema.

Daktari anena

Dk Suleiman Abdul Ali, mratibu wa huduma za afya mjini wa Hospitali ya Kidongo Chekundu alikotibiwa msichana huyo, alisema wanaendelea na uchunguzi wa afya ya akili ya msichana huyo.

Dk Ali alisema wamempatia dawa na wazazi wake wametakiwa kutozungumza naye kuhusu tukio hilo na wanaendelea kushirikiana na familia ya msichana huyo ili kuona hali ya afya yake.

 

Ni mjuzi wa kuogelea

Picha za video zinamuonyesha msichana huyo akiwa amejiweka kwa jinsi ambayo anaelea juu ya maji kama mtu ambaye anajua mbinu za kukabiliana na maji.

“Tangu akiwa mdogo amekuwa na mazoea ya kwenda kuogelea baharini pamoja na wenzake. Nyumba wanaoishi ipo takriban mita 600 kutoka baharini,” alisema Manzi.

Mwananchi

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364