-->

Uchaguzi kesho Kenya,milipuko yatokea

Wakati Wakenya wanapiga kura kesho kuchagua kiongozi wa nchi yao, limetokea shambulio linalodaiwa la kigaidi kwa kulipuliwa nguzo ya umeme mkubwa wa kilovoti 220 na kusababia kuzima kwa umeme katika kisiwa cha Lamu na maeneo mengine ya Mpeketoni.


Shambulio hilo lilitokea jana asubuhi lilisababisha kukosekana kwa umeme katika kisiwa hicho na maeneo ya jirani. Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Umeme, Dk Ken Tarus alisema ni kitendo cha kigaidi na mfundi walikuwa tayari eneo la tukio kurejesha umeme.

Uchaguzi huu unafanyika huku Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ikiwa imetangaza idadi ya walio kwenye daftari la wapiga kura ambao wanafiki 19,687,563 kukiwa na ongezeko la wapiga kura milioni 3.8 wengi wakiwa vijana wenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 34.

Mbali na idadi ya wapiga kura, IEBC pia kuongeza vituo vya kupigia kura kutoka 31,000 vya awali hadi vituo 45,000, lengo kila kituo kiwe na wapiga kura wasiozidi 700 ili kuharakisha zoezi la kupiga kura na kuhesabu.

Pamoja na ongezeko la vituo hivyo 14,000 vya kupigia kura, pia IEBC ilifuta majina ya wapigakura 80,000 ambao kwa maelezo ni wale waliofariki dunia.

Upigaji kura

Vituo vya kupiga kura vitafunguliwa kuanzia saa 12 asubuhi na Rais Uhuru Kenyatta atapiga kura kwenye Shule ya Msingi Mutomo iliyoko Gatundu South, Kiambu. Shule hiyo imeelezwa kukarabatiwa siku chache zilizopita ili iwe na muonekano mzuri na kwa heshima ya kiongozi huyo.

Shule hiyo ilifanyiwa ukarabati wa kupakwa rangi kwenye kuta zake ikiwamo kurekebishwa mifumo ya umeme kwa gharama ya Sh15,000. Kituo ndicho kilichotumiwa na Uhuru kupiga kura katika uchaguzi uliopita uliomuweka madarakani.

Mpinzani mkuu wa Uhuru, Raila Odinga anayegombea kupitia chama cha Orange Democratic Movement (ODM), anapiga kura kwenye eneo la Kibra, maeneo yote hayo yapo jijini Nairobi.

Naibu Rais, William Ruto ambaye ni mgombea mwenza wa Uhuru, atapiga kura huko Sigoi, Uansin Gishu katika mji wa Eldoret, ,mgombea mwenza wa Odinga, Kalonzo Musyoka yeye anapiga kura katika eneo la Tseikuru huko Kitui.

Mbali ya kulipuliwa nguzo ya umeme huko Lamu, baadhi ya vigogo wa National Super Alliance (Nasa), Musalia Mudavadi na mgombea ugavana wa Mombasa, Ali Hassan Joho, jana asubuhi kwa nyakati tofauti na maeneo tofauti walizungumza na vyombo vya habari kutoa malalamiko yao kuhusu kusambazwa wanajeshi.

Joho aliwaita waandishi wa habari mjini Mombasa na kuwaambia ameona wanajeshi wakisambazwa uwanja wa ndege bila kuelezwa sababu, pia alidai ana wasiwasi leo pamoja na wanasiasa wengine wa upianzani watakamatwa na polisi.

Akizungumza jijini Nairobi, Mudavadi alidai wamepata taarifa kutoka kwa mmoja wa wasaidizi wa Inspekta Jenerali wa Polisi, kwamba ndege yenye namba Y12 iliruka kutoka katika kambi ya anga ya jeshi iliyopo Laikipia ikiwa imebeba masanduku makubwa sita yakiwa na silaha za kutungula ndege za gurumeti.

Mudavadi alidai nusu ya masanduku hayo yalishushwa Nairobi na yaliyosalia yalishushwa Lamu. Hata hivyo Jeshi la Polisi lilitoa taarifa kwamba limezungumza na viongozi hao ambao nao walitoa taarifa kwamba wameridhika na sababu zilizitolewa na polisi kwamba askari hao hawapelekwi kwenye masuala ya dharura.

Wakati Mudavadi na Joho wakitoa madai hayo, mgombea urais wa Nasa Raila Odinga jana alikutana na baadhi ya wajumbe wa Bunge la Ulaya ambao wamo kwenye kundi la waangalizi kutoka Umoja wa Ulaya, ambapo aliwalalamikia kwamba IEBC imeshindwa kutoa nakala ya orodha ya walioandikishwa kupiga kura licha ya kulipia ada ya kisheria ya Sh20,000.

Huko Nyeri kwenye uwanja wa mpira wa Dedan Kimathi, Kanisa la Mt Kenya liliandaa maombi maalumu kwa ajili ya uchaguzi wa leo yaliyoongozwa na Askofu wa Kanisa Katoliki, Anthony Muheria. Maombi hayo yalihusu kuliombea Taifa lipite salama katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Kaunti ya Kwale mgombea wa Wiper, Ali Chiran Mwakwere ametoa malalamiko kwamba kuna watu wanasambaza ujumbe kuwa amejitoa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi na ameitaka IEBC kufanya uchunguzi wa haraka.

Wakati Mwanakwere akilalamika, mgombea binafsi katika kaunti hiyo, Sammy Ruwa yeye ametangaza kukubali matokeo yatakayotolewa IEBC, huku mgombea mwingine wa Kaunti ya Mathira mgombea wa Jubilee, Rigathi Gachagua yeye ameipongeza IEBC kwa kufanya maandalizi mazuri ya uchaguzi.

Uchaguzi huu kwa mara kwanza utawarusuhu wafungwa walio gerezani kupiga kura, ambapo jana walikuwa wakiandaliwa kwa kupewa maelekezo na maofisa magereza wa namna ya kupiga kura. Kura watakayopiga ni rais pekee kwa kuwa wao jela siyo makazi yao ya kudumu.

Kiongozi wa kundi la waangalizi kutoka Kituo cha Jimmy Carter, John Kerry ameeleza kuridhishwa na maandalizi ya uchaguzi na kwamba sasa ni kazi kwa Wakenya kuchagua kiongozi wao.

Kerry ambaye aliwahi kugombea urais wa Marekani na pia ni waziri wa zamani wa mambo ya nje chini ya uongozi wa Rais Barack Obama, alisema anatumaini uchaguzi utafanyika kwa amani, tulivu na uwazi.

Naye mwangalizi kutoka Senegal, Dk maina Toure alisema kwa namna alivyofuatilia mchakato wa uchaguzi, anaamini hali itakuwa shwari na hakutakuwa na vurugu kama hofu ilivyotanda kwa wengi.

Wakati viongozi hao wakisema hivyo, Kaimu Waziri wa Usalama, Dk Fred Matiang’i jana awahakikishia wananchi wa Kenya kwamba hakutakuwa na vurugu na yeyote aliyepanga kuvuruga uchaguzi hawatamvumilia.

Aliwataka Wakenya kutoka kwa wingi na bila hofu kwenda kupiga kura kwa kuwa ulinzi upo wa kutosha na uchaguzi utafanyika kwa amani na utulivu.

Wasemavyo wananchi

Baadhi ya wakadhi wa Kericho wanaamini uchaguzi wa leo utakuwa wa amani kuliko uchaguzi wa mwaka 2013. Licha ya eneo hilo la Kericho kuelezwa ni miongoni mwa maeneo yenye vurugu watu wengi wamesema watapiga kura asubuhi na baadaye watakwenda kwenye shughuli zao za kawaida.

Kennerth Tirop ambaye kazi yake ni kung’arisha viatu alisema hali inaonekana ni shwari na yenye amni. “Hakuna dalili za kutokea vurugu wala mapigano,” alisema.

Dereva wa bodaboda, Evans Rotich na muuuza duka Sally Koech kwa pamoja walisema mazingira ni tulivu na kuondoka kwa watu hasa wasio wenyeji kwa kurejea kwao ni suala la kawaida.

Hata hivyo, naibu kamanda wa polisi katika eneo la Kericho East, Stanslaus Apwokha alisema kutakuwa na polisi wawili katika kila kituo cha kupigia kura na aliwahakikishia wananchi kwamba hali itakuwa ya usalama.

Mkazi wa Kwale, Mwanakombo Mwaleso alisema anatumaini hakutakuwa na vurugu kwa kuwa kampeni zilifanyika kwa amani na salama. Mkazi mwingine Hamza Swaleh alisema ametiwa matumaini na maandalizi yaliyofanywa na IEBC.

“Hakuna tukio lililoripotiwa katika Kaunti na tunategemea uchaguzi ulio huru na amani na kwamba hali hii itakuwa imeibadilisha nchi,” alisema.

Mkazi mwingine kutoka jimbo la Msambweni, Kisuse Hassan aliwataka wenzake kutambua umuhimu wa kuiombea nchi amani.

“Nataka kuwaeleza Wakenya watumie haki yao ya kidemokrasia lakini pia watilie maanani umuhimu wa amani katika kuliendeleza Taifa,” alisema.

Pia, aliwataka polisi kutotumia nguvu kupita kiasi pale wanapopambana na watu waliovunja sheria.

Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima cha Laikipius, Martin Evans alisema anaamini Wakenya watapiga kura kwa amani wakati wa kuchagua viongozi wanaowataka.

Kwa upande wake Felister Moiyare alisema wakazi wa eneo hilo watachagua kiongozi wanayempenda ambaye atawahakikishia amani na utulivu.

Wakazi wa Nairobi walisema macho yao yko kwenye matumizi ya mfumo wa kielectroniki wa mtandao utakaotumika kutuma matoke ambao ndio kama utatumika vizuri maana yake uchaguzi utakuwa wa haki.

“Nairobi hatutegemei tatizo la mitandao tunategemea kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Vitalis Otieno.

 Mwananchi

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364