-->

Ushindani Wanaoukataa ‘Bongo Movie’ Umewapaisha Bongo Fleva

KADRI siku zinavyokwenda ndivyo tasnia ya filamu inaonekana kudumaa huku muziki wa Bongo Fleva ukionekana kuzidi kukata anga. Achana na Diamond, Ali kiba na Vanessa Mdee, Bongo Fleva ina vichwa vingi vinavyoweza kuwa kielelezo cha ubora wa muziki wao.

Ndani ya Bongo Fleva kuna Jux, Mr Blue, Barakah Da Prince, Kasim Mganga, Ney wa Mitego, Darassa, AY na wengineo lukuki. Hawa wote wanafanya vizuri. Hali hii ni tofauti sana na kilichopo kwenye tasnia ya filamu.

Kwenye filamu wasanii walio juu kwa maana ya kufanya vizuri kiuhalisia hawazidi watano. Hii siyo afya kwa tasnia inayohitaji kukua. Tasnia yoyote makini ili ikue inahitaji iwe na ushindani wa kutosha.

Hali ya kuwa na staa mmoja ama wawili katika tasnia ya filamu inachangia tasnia ikose msisimko kwa kuwa katika hao wawili ama watatu wanaotamba kila siku wanakuwa na mawazo yale yale hivyo kukosa ushindani unaowafanya waumize vichwa zaidi. Hali hii isipobadilika, sioni kama tasnia hii itakuja kufanya vizuri.

Wengi wanasema marehemu Steven Kanumba kaondoka na msisimko wa filamu. Kwa upande fulani nakubaliana na hoja hiyo kutokana na mazingira halisi. Ila ukweli mchungu ni kuwa hata kama Kanumba angekuwa hai mpaka leo, tasnia hiyo ingepoteza mvuto tu kwa jamii.

Unadhani ni kwa namna gani wasanii wawili waweze kuleta ushindani unaostahili katika fani miaka yote? Hapana.

Kutamba kwa Kanumba na Ray katika zama zile ilikuwa ni kwa sababu ya wengi kuona filamu za namna ile kama kitu kigeni hivyo kujikuta wakibabaishwa na ugeni huo. Ila ugeni usingekuwapo mpaka sasa.

Bongo Fleva imeweza kutishia heshima ya miziki mingine inayotamba Afrika kwa sababu wasanii wanaotamba ni zaidi ya kumi. Kwa mfano katika shoo kama Fiesta wasanii mastaa wa ndani wanakuwa zaidi ya 20, kwa namna hii unadhani Bongo Fleva itaacha kutamba?

Ili Bongo movie iweze kusogea, inabidi watu wathaminiwe kutokana na vipaji na ubora wa hadithi zao. Sura, maumbile na ustaa wa mtu inafaa isiwe kigezo muhimu cha mtu kupewa nafasi katika filamu kama hana uwezo.

Bahati mbaya sana katika tasnia hii, ni kuwa wasanii wakali wapo wengi, ila hawana uwezo wa kumudu vifaa vya kisasa kama iliyo wale wababaishaji wenye sura na maumbile yanayowavutia waongozaji hivyo kushindwa kuleta ushindani unaotakiwa.

Ubinafsi na umwinyi unaonekana kuwepo kwenye tasnia hii unachangiwa kwa asilimia kubwa na kushindwa kushikana mikono (kusaidiana) kwa imani kuwa mmoja akimsaidia mwenzake kutamba basi hii ndiyo itakuwa mwisho wa ustaa wake.

Mawazo haya sio tu ya kijinga ila pia ni sumu katika maendeleo ya filamu zetu.

Waige mfano kwa Diamond ambaye kamchukua Rich Mavoko na kamsainisha mkataba kwenye lebo yake. Rich Mavoko huyu ni msanii ambaye kwa miaka kadhaa alitajwa kuwa mshindani halisi wa Diamond kutokana  na ubunifu na kipaji chake ila yeye hakujali hayo, kamsogeza karibu ili wapige kazi.

Kwa moyo na uamuzi huu wa Diamond unadhani Bongo Fleva itashuka? Ngumu sana.

Ili tasnia ya filamu inyanyuke ihitajika wasanii wabadili fikra, watokwe na dhana za kubaniana na washirikiane kwa pamoja ili kurudisha hamasa ambayo tayari imepotea.

Kila msanii afahamu kuwa kama ana kipaji halisi hana haja ya kuhofia ushindani. Ushindani siyo tu utakuza tasnia ya filamu na kuipa thamani kubwa ila pia utamfanya hata yeye akue zaidi kwa kuhofia kupitwa. Mtu yoyote anayeogopa ushindani hana nafasi ya kukua.

Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364