VIDEO: 80% Bongo Movie Hawana Vipaji – Aunty Ezekiel
Msanii wa filamu nchini Tanzania Aunty Ezekiel amefunguka na kusema kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wasanii wa filamu nchini hawana vipaji, na wanafanya kazi kiubabaishaji, jambo linalochangia tasnia hiyo kuporomoka.
Aunty amesema hayo alipokuwa kwenye kipindi cha Kikaangoni kupitia ukurasa wa Facebook wa EATV, na kusema kuwa sehemu kubwa ya wasanii wa filamu nchini hususani wenye majina makubwa, wanashindwa kufikia malengo yao, na malengo ya tasnia kutokana na kukosa vigezo.
Huku akisita kuwataja majina, amesema kuna baadhi ya wasanii hususani wa kike, wameingia kwenye tasnia hiyo kwa lengo la kutafuta umaarufu ili waonekane kwa aina fulani ya watu kwa malengo tofauti, huku wengine wakishindwa kutoa kazi za filamu lakini bado wanajiita wasanii wa filamu.
Wasanii wengi sana wameingia kwenye tasnia hawana vigezo na ndiyo maana kila siku wanafanya kazi lakini hawafiki popote, kuna wengine wanaingia kwa ajili ya kutafuta umaarufu, unakuta mwingine ananifuata anasema anataka kuwa maarufu kama mimi, sasa huyo amekuja kufanya kazi au kutafuta umaarufu?. Amehoji Aunty.
Aunty ameendelea kusema “Kuna wengine tayari wameshapata vijina, lakini hawana vigezo, kama asilimia 80 hivi hawana vigezo labda asilimia 20 tu ndiyo watu ambao wako perfect”.
KANUMBA HAJAUA BONGO MOVIE
Vilevile Aunti Ezekiel amewaeleza wadau wa bongo movie kuwa siyo kweli kwamba marehemu Steven Kanumba amekufa na tasnia yake huku akisema tatizo lipo kwao wenyewe wasanii.
Amebainisha hilo kutokana na minong’ono mingi kuenea kuwa tokea Kanumba kufariki na filamu imekosa changamoto pamoja na ubunifu kabisa mpaka kupelekea wadau kupenda kazi za nje ya nchi.
“Si kweli kwamba marehemu Kanumba amekufa na bongo movie yake ila tatizo lipo kwetu wenyewe kwa waigizaji kukosa muda wa kutengeneza kazi nzuri kama ilivyokuwa awali”.
AMZIMIA GABO ZIGAMBA
Vile vile Anti alimpongeza Gabo Zigambo kwa kufanya kazi nzuri na kusema huyo kwa sasa ndiye mwanaume wa pekee mwenye nafasi ya kuziba pengo aliloliacha Kanumba labda yeye mwenyewe asitake kufika hatua hizo, lakini akasema kuwa kinachomuangusha kwa sasa ni kuyumba kwa tasnia yenyewe.
“Kama bongo movie ingekuwa haijayumba Gabo ndiye angeweza kuchua nafasi ya Kanumba, nampenda kwa kazi kazi zake”
Kwa upande mwingine Aunty amesema ana mpango wa kuanzisha lebo yake ya movie kwa ajili ya kuendeleza vipaji vya uigizaji nchini lakini kwa kuwa sasa mambo si shwari, anasubiri tasnia ya filamu ikae vizuri ili atekeleze malengo yake.