Wananiroga Sana – PNC
Msanii PNC ametoa sababu ya yeye kutofanya vizuri sasa hivi kwenye kona ya muziki, huku akihusisha imani za kishirikina, ambazo hivi karibuni baadhi ya wasanii wamekiri kuwepo kwa mambo hayo.
PNC ameyasema hayo alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa Radio, na kusema kuwa pamoja na kuwa ameshawahi kufanya kazi zingine tofauti na muziki, ana imani anafanyiwa figisu figisu za kishirikina.
“Wananiroga kweli kweli, mi nimetoka maisha ya local kabisa, mimi nimeshawahi kuwa hata mchunga ng’ombe mchunga mbuzi, nishakuwa muwindaji, maisha yetu yale ni ya dhiki, kwa hiyo yani asije mtu akafikiria labda tunamuona anahangaika hangaika, anakomaa kutoa nyimbo kwa sababu labda anataka tu ajitutumue kufanya kitu kimsaidie katika maisha”, alisema PNC.
Pia msanii huyo ambaye kwa sasa ana wimbo mpya unaoitwa ‘ekotite’ amesema hata akiendelea kutoa muziki na kutofanya vizuri, hatoacha kwa sababu ki kitu ambacho anakipenda.
“Na hata nikifeli muziki niko tayari kufanya kitu chochote, nafanya muziki kwa sababu naupenda”, alisema PNC
eatv.tv