-->

Wasanii wa Bongo Muvi Waandamana Kariakoo Dar (+Video)

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda akishirikiana na Wizara ya Habari pamoja na wasanii wa filamu wameendesha operesheni maalum katika mitaa ya Kariakoo Jijini Dar es salaam kwa dhumuni la kupambana na wazalishaji wa CD ‘feki’ za filamu kutoka nje ya nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda akiwa katika operesheni hiyo Kariakoo Jijini Dar es salaam.

Hatua hiyo imekuja baada ya wasanii wa filamu nchini kumtembelea RC Makonda na kulalamika juu ya filamu hizo za nje kwa madai zimekuwa zikiwaharibia biashara kwa kuwa zinauzwa kwa bei ndogo na pia hazilipi kodi, ilhali wao wanalipa. RC alitoa siku 10 ambazo zimemalizika jana kwa wazalishaji pamoja na wauzaji wa CD feki kuacha biashara hiyo huku akiwataka wale wenye uwezo kufanya biashara hiyo kufuata taratibu halali za kibiashara.

Akiongea na wafanyabishara hao wakiwa wamefunga maduka yao, RC Makonda amesema hana lengo la kukataza filamu za nje ziuzwe nchini, ila watu ambao wanafanya biashara hiyo wanatakiwa kufuata taratibu kama ambavyo wasanii wa filamu wa ndani wamekuwa wakifanya katika filamu zao.

“Yule anayesambaza na kuzizalisha ndiye ambaye tunamhitaji. Nyie wafanyabiashara tumewaandalia utaratibu wa vitambulisho kutoka Bodi ya Filamu ambavyo vitafanya mtambulike, kwa sababu hakuna biashara isiyotambulika duniani,” alisema RC Makonda. “Hivi vitambulisho vitakuwa na madaraja, mkionana na wahusika wa Bodi ya Filamu watawaelezea nini cha kufanya. “Wale wenye mitambo ya kuzalisha wapo 13 tukutane Polisi Central Jumatatu mkiwa na CD zenu,”

“Hivi karibuni Mh Waziri hapa bandarini alifanikiwa kukamata kontena zenye CD za nje zenye thamani ya shilingi bilioni 4. Wale watu wakawa wanasema ni empty CD, kuja kuzikagua tukakuta zina content ndani. Kwa hiyo lengo letu sio kuwazuia kufanya biashara, bali tunataka mfanye biashara lakini kwa kufuata taratibu zote. leo nimekuja na maafisa 200 wa TRA ambao watazunguka kwenye maduka mbalimbali kuangalia kama watu wanalipa kodi, kwa hiyo kama uko hapa na unajua mambo yako hayapo sawa nakuomba kabisa uwatafute wahusika wakuambie nini unatakiwa kufanya,” aliongeza RC Makonda.

Kwa upande mwingine, mmoja kati ya wafanyabishara aliyejitambulisha kwa jina la Salim Majonjo, amedai wanapata wakati mgumu kuuza kazi za wasanii wa Bongo Movie kwa madai kua hazina ubora na zinazungumzia mapenzi zaidi, ndiyo maana ameamua kugeukia kwenye soko la filamu za nje.

“Mh atufikirie na sisi wafanyabiashara wadodo wadogo, sisi ndo tunajua hali ya soko la filamu likoje. Ni filamu chache za Bongo ambazo unaweza ukauza tena zinahesabika. Yaani unaweza kukaa toka asubuhi mpaka jioni na usiuze filamu hata moja lakini filamu za nje zikawa zinatembea muda wote, stori zao kila siku zile zile watu wanachoka. Lakini ukileta filamu ya marehemu Kanumba inauza tena sana. Jiulize kwanini hao filamu zao haziuzi. Mimi ningewashauri wafanye kazi nzuri ambazo zitawavutia mashabiki wao huo ndio utakuwa muarobani wa hicho wanachokizungumzia,” alisema mfanyabiashara huyo.

Mmoja kati ya wasanii wa filamu ambao walikuwa katika opereshini hiyo, Rado, ameishukuru ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda, kwa hatua hiyo huku akiwataka Watanzania kwa ujumla kuwaunga mkono.

“Kwanza namshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam kwa hatua hii nzuri, sisi kama wasanii tunatambua juhudi za serikali katika kuhakikisha wasanii wananufaika na kazi zao, na pia serikali inapata kodi yake. Kila msanii analipa kodi kupitia movies zetu, kila movie ikiuzwa asilimia 30 inaenda kwa serikali, kwa hiyo mnaona ni namna gani tunalipa kodi. Sisi tunataka na hawa ambao wanaingiza fulamu za nje walipe kodi kama sisi kwa sabubu wote tunatumia soko moja tena mbaya zaidi wao filamu zao wanauza kwa bei ya chini zaidi,” alisema Rado.

Muigizaji huyo amewataka wasanii wenzake wa filamu kuendelea na vita hiyo ili kahikikisha wananufaika na kazi zao.

Bongo5

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364