Wastara Atengwa Bongo Muvi
DAR ES SALAAM: Baada ya staa wa sinema za Kibongo, Wastara Juma kufunga ndoa na mheshimiwa Sadifa Juma, anadaiwa kutengwa na wasanii wenzake wa Bongo Muvi hasa wale waliokuwa karibu naye katika zoezi la kumchangishia fedha za matibabu aliyokuwa akitarajia kwenda kuyafanyiwa nchini India.
Sosi wa ndani ya Bongo Muvi alilinyetishia Ijumaa kwamba, baadhi ya mastaa walifikia uamuzi kufuatia kukasirishwa na kitendo cha Wastara kuolewa ghafla bila kuwashirikisha wao.
“Wasanii wamemkasirikia sana Wastara na ninavyokwambia kwa sasa kimenuka kwani hawataki hata kumsikia.
“Wanamshangaa kuolewa wakati anaumwa na alikuwa akiomba msaada hivyo wamemtenga na wamesitisha michango yake,” kilifunguka chanzo hicho.
Ilielezwa kwamba, aliyekuwa akiongoza ishu ya kumchangishia ni Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Simon Mwakifwamba aliyejitolea kuandika barua na kuipeleka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa ajili ya kuomba msaada wa matibabu ya mguu wake nchini India lakini walisitisha mara moja zoezi hilo baada ya ndoa hiyo.
Mwakifwamba alipoendewa hewani na kufikishiwa ishu hiyo alisema: “Nilifuatwa na kaka wa Wastara, akaniomba kuwa dada yake anaumwa sana, anahitaji kwenda kwenye matibabu India, nikaamua kumuandikia barua ya kumuombea msaada wizarani.
“Barua hiyo niliipeleka kwa katibu mkuu wa wizara hiyo, Profesa Elisante Ole Gabrielleo. Alipoipokea aliniambia kuwa ataishughulikia iende Wizara ya Afya kwa ajili ya matibabu hayo haraka na mchakato ulikuwa unaenda vizuri.
“Ilipofika jioni nikashangaa kuona mitandaoni kuwa Wastara anaolewa, nikaona nimpigie haraka katibu mkuu kwani barua yangu ilisema kuwa Wastara ni mgonjwa sana ambaye anahitaji matibabu ya haraka kwa hiyo kitendo cha kufunga ndoa kilinishtua kwani sikulitambua.
“Baada ya kumweleza katibu mkuu huyo alisema kuwa kwa sababu ameolewa na mbunge kuna taratibu zao azifuate hivyo tukaishia hapo.”
Kwa upande wake Wastara alifunguka mambo mazito ya kusikitisha: “Nikiongea sasa nitaonekana najitetea lakini wasanii wenzangu wajue kuwa niliamriwa na mume wangu, niliwatumia ujumbe kwenye makundi yetu na kuwaeleza kuwa naolewa.
“Hata hivyo, ndoa haikuwa imepangwa kwa siku hiyo kama wanavyodhani ila baada ya mimi kuwa na hali mbaya, Sadifa aliwaomba ndugu zangu na kuwaambia kuwa anataka anioe hivyohivyo ili anihudumie kwa sababu tulipanga ndoa baada ya mimi kutoka kwenye matibabu.
“Wasanii ni watu wa kulaumu tu, ila mimi naumwa sana, Mungu akipenda nitakuwa India ‘soon’, nitafanyiwa matibabu na anayetaka kunichangia nitamshukuru.”
Chanzo: GPL