-->

Wema Amlipua Mke wa ‘Nabii’ Tito

DAR ES SALAAM: Katika hali isiyotarajiwa, imeelezwa kuwa msanii nyota wa filamu za Kibongo, Wema Sepetu, amemlipua mke wa ‘Nabii Tito’ baada ya mwanamke huyo kumshawishi kupitia mitandaoni aolewe na nabii huyo.

Chanzo chetu makini kilisema kuwa, msanii huyo amekasirishwa na kitendo cha mke huyo kumshawishi kuolewa na mumewe anayeitwa Onesmo Machija ‘Nabii Tito’ (44).

“Wema Sepetu nakupenda sana hata Nabii Tito anakupenda sana, kwanza mzuri, una shepu nzuri hata katika mambo ya Kiafrika unaongoza kwa uzuri.

“Nabii Tito huyo kwa watu wasiomfahamu wanasema sio nabii lakini kwa mimi ninayemfahamu na kuishi naye naona mambo ya kinabii anayofanya, nakuomba ukubali hata mimi nakupenda sana, kwanza una shepu nzuri.

“Uwe mke mwenzangu, ukubali kuwa mke wa Nabii Tito. Sikia kilio cha mke wa nabii,” amesikika kwenye video mke huyo wa Nabii Tito akimbembeleza Wema.

Naye Nabii Tito kwenye video hiyohiyo amechombeza kwa kubembeleza kwamba Wema akubali kuwa mkewe ili kanisa lao likuwe.

Nabii Tito na mkewe

Alipotafutwa Wema na kuulizwa kuhusiana na video hiyo alisema, ameiona na amekasirishwa na kile walichokifanya nabii huyo na mkewe.

“Kiukweli wameniudhi sana kwa kunidhalilisha. Nawasiliana na mwanasheria wangu ili nimburuze mahakamani mwanamke huyo,” alisema Wema.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi mkoani Dodoma, mapema wiki hii lilimkamata nabii huyo na kumfanyia mahojiano kutokana na mahubiri ya kidini anayoyafanya na limesema mtu huyo ana matatizo ya akili.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, SACP Gillesi Muroto amesema Juni 23, 2014, mtu huyo aliwahi kulazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu ya akili chini ya daktari aliyejulikana kwa jina moja la Dk. William ambapo aliporuhusiwa alitakiwa kurejea hospitalini hapo Julai 9 mwaka huohuo lakini hakurejea.

Kamanda Muroto aliendelea kusema kwamba, baada ya hapo Machija ambaye kanisa lake halijasajiliwa popote, aliibukia mkoani Dodoma katika Kijiji cha Nong’ona kilicho karibu na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) akifanya mahubiri ya kidini yaliyodaiwa kuwa hayakuwa na maadili ya kidini.

“Kwa msingi huo, jeshi la polisi limempeleka Hospitali ya Rufaa ya Milembe iliyoko mkoani Dodoma kwa ajili ya kumpima tena matatizo hayo ya akili na baada ya majibu kutolewa, Dk. Dixon Philipo aliyemshughulikia alithibitisha kwamba bado ana matatizo hayo ya akili,” alisema kamanda Muroto juzi na kusisitiza kuwa wanaendelea kumshikilia kutokana na matendo yake aliyoyafanya ili kufanya uchunguzi zaidi.

Chanzo:GPL

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364