Wema, Petit Ndani ya Bifu
Imevuja! Urafiki wa muda mrefu wa muigizaji nyota, Wema Sepetu na mshika kamera wake, Petit Man umeingia dosari baada ya kudaiwa kuwa wawili hao wako ndani ya bifu, Risasi Mchanganyiko linakujuza.
Chanzo makini kililiambia gazeti hili kuwa Wema na Petit ambao hapo awali walikuwa wakiambatana kama kumbikumbi, kila kona walipoonekana, hivi sasa ni kama paka na panya kwani hakuna mawasiliano kati yao.
“Wema na Petit hali ya hewa imechafuka, kwa sasa hawaongei kabisa kwa sababu Muna ambaye ni rafiki yao wote anadaiwa kumwambia maneno yaliyomkasirisha madam kuhusu mpigapicha huyo na kusababisha bifu hilo kali,” kilisema chanzo hicho.
Baada ya kupata ubuyu huo, gazeti hili liliwatafuta wahusika na wa kwanza kupatikana alikuwa Petit Man, aliyekiri kuchafuka kwa hali ya hewa.
“Unajua mimi na Wema nipo naye kwa miaka tisa sasa na ni kama familia moja, hivyo tatizo lililopo kati yetu litaisha tu na kumalizwa kifamilia kwa hiyo watu wasilivalie sana njuga,” alisema.
Kwa upande wake Muna ambaye ni rafiki wa wote wawili, alisema anasikia watu wakizungumza kuhusu kuwagombanisha Petit na Wema, kitu ambacho alidai siyo kweli, kwani hawezi kuwagombanisha watu ambao ni kama ndugu na kwamba yupo tayari kusawazisha matatizo kati yao badala ya kuchochea.
“Mimi kwa kweli nawashangaa watu wanaosambaza hayo maneno ni kwa vile tu hawajui, mimi siwezi kuwagombanisha wale ni familia moja, waligombana kwa ishu zao wenyewe, sihusiki nazo na mara nyingi ninachofanya kama wana tatizo huwaweka sawa ili waendelee na uhusiano mzuri na si kuwagombanisha,” alisema Muna.
Lakini jitihada za gazeti hili kupata kauli ya Wema zilishindikana baada ya simu yake ya mkononi kuita bila kupokelewa hadi linaingia mitamboni.
Chanzo:GPL