-->

Wema Sepetu Aibua Mtandao wa Diamond Unaomgonganisha na Marafiki, Ndugu

DIAMOND Platnumz bado moto. Anaendelea kutengeneza headline kwenye vyombo vya habari vya ndani na nje ya Bongo. Magazeti, redio, televisheni na hata mitandao ya kijamii havina uwezo wa kumkwepa.

 

Anaandikika. Wakati juzi usiku akidondosha singo yake mpya inayokwenda kwa jina la Hallelujah ambayo amefanya kolabo na Morgan Heritage, kundi la Wajamaika walioshinda Tuzo ya Grammy mwaka jana kwenye kipengele cha Album Bora ya Reggae, mpenzi wake zilipendwa, Wema Sepetu alikuwa akisherehekea sikukuu yake ya kuzaliwa.

Alizaliwa Septemba 28, miaka kadhaa iliyopita. Wema, staa ambaye aliibuliwa na shindano la Miss Tanzania 2006 ndiye mrembo pekee kutoka Miss Tanzania ambaye ameendelea kuwa maarufu na kutengeneza habari kwa miaka zaidi ya kumi mfulululizo.

Mrembo aliyemtangulia Nancy Sumari (Miss Tanzania mwaka 2005) pamoja na mafanikio makubwa aliyopata kwenye mashindano hayo hadi kuibuka Miss World Africa 2005, hajafua dafu kwa Wema kwa umaarufu na kukubalika kwenye jamii.

Kwa umaarufu, ushawishi na kukubalika kwake, watu mbalimbali ndani na nje ya nchi walimtakia heri ya siku yake ya kuzaliwa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii na hasa ule unaotumiwa na mastaa wengi zaidi nchini Instagram.

Miongoni mwa mastaa waliomu-wish happy birthday ni pamoja na Nasibu ‘Diamond’ Abdul, Esma Platnumz, dada wa Diamond na Hamisa Mobetto, mzazi mwenzake na Diamond.

Pengine salamu kutoka kwa marafiki na wadau wengine wote zilionekana za kawaida tu, ila pongezi za mastaa hawa ambao wana uhusiano kwa namna moja ama nyingine, zimeibua mtungo wa kiuhusiano aliopata kuwa nao au kuelezwa kuwa nao msanii Diamond.

Hapa chini Swaggaz inakuletea mtungo ambao unamhusisha Diamond na watu wake wa karibu kishkaji na hata kinasaba.

DIAMOND > WEMA > IDRIS

Akimtakia heri ya kuzaliwa, Diamond aliandika kwa kifupi sana: “Happy birthday Madam….” ambapo katika andiko lake hilo, alisindikiza na picha ya pozi aliyopiga na Idris Sultani, komediani ambaye uhusiano wake na Wema ulikuwa official na wenyewe waliweka wazi.

Haijajulikana kama uhusiano wao bado una uhai, maana siku za hivi karibuni kumekuwa na minong’ono kuwa Wema anatoka na mwanamume mwingine ambaye siyo maarufu. Swaggaz halina uthibitisho wa hilo, hivyo linaacha kama madai tu.

Kuhusu Wema na Diamond, siyo stori – mambo yanajulikana kuwa waliwahi kupika na kupakua. Wadadisi wa mambo wanasema Diamond aliamua kuposti picha ya Wema akiwa na Idris ili kuzima soo kwa mpenzi wake wa sasa Zarina Hassan ‘Zari The Boss Lady’ ambaye huenda wishes yake ikafikiriwa vibaya kwamba amekumbuka enzi zao za zilipendwa!

DIAMOND > HAMISA > PETIT > ESMA

Kwa sasa hakuna ubishi wowote kuhusu Diamond kutoka kimapenzi na mwanamitindo Hamisa Mobetto na kuzaa naye mtoto Dylan au Abdullatif kama ambavyo Hamisa anapenda aitwe.

Diamond amekiri kuwa alikuwa na uhusiano na Hamisa muda mrefu, kabla hata hajaingia kwenye mapenzi na Wema, lakini wakaachana na baadaye kulianzisha tena walipokutana kwenye kibao cha Salome.

Hamisa amewahi kuwa na uhusiano na Petit Man ambaye kwa sasa anatoka na Esma Platnumz aliye dada wa Diamond! Unaweza kuona huo mtungo hapo ulivyo.

Tayari picha zinazowaonyesha Hamisa akiwa na Petit Man kimalavidavi zimeshasambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, lakini Esma amevunja ukimya na kuzitolea ufafanuzi ambapo aliandika:

“Semeni mtakuja kunyamaza kisha mwisho mtakuja kusema mpaka Daylan ni mtoto wa Petit Man, basi wekeni na picha ya Hamisa na Petit Man wakiwa kitandani.”

Lakini akitoa heri ya kuzaliwa, Esma aliandika: “Heri ya kuzaliwa tena na kuona siku nyingine tena Mungu akupe maisha marefu na furaha tele ndani yake…”

Hamisa yeye aliandika: “Happy birthday Da Wema.
Nakupenda sana….mengine ntakwambia inbox .”

DIAMOND > WOLPER > HARMONIZE

Wakati akianza kuvuma kisanii, staa wa kwanza kutoka na Diamond na uhusiano wao kuwa official ni mwigizaji Jacqueline Wolper lakini uhusiano wao haukudumu muda mrefu wakaachana.

Diamond alipoachana na Wolper aliendelea na hamsini zake, lakini baadaye ukaja kuanzishwa uhusiano kati ya mtoto wa Kichagga Wolper na kijana wa Kimakonde, Msafi Harmonize kutoka Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) ambayo Diamond ndiye mkurugenzi.

DIAMOND > WEMA > KAJALA

Siyo Diamond wala Kajala Masanja waliowahi kukiri uhusiano huo hadharani lakini inaelezwa kuwa Diamond aliwahi kupita kwa Kajala japo hakukaa kwa muda mrefu.

Ikiwa hayo yana ukweli, basi tayari wanaingia kwenye mtungo unaowakutanisha na Wema ambaye alipata kuwa shosti wa karibu na Kajala.

Madai ya chini kwa chini yanasema kuwa, chanzo cha bifu la Wema na Kajala hadi kufikia hatua ya kila mtu kuendelea na hamsini zake ni Kajala kuingilia uhusiano wake na Diamond.

Diamond alipata kufafanua madai hayo kwenye gazeti moja linalotoka mara moja kwa wiki, akidai ni madai kama yalivyo madai mengine mengi anayohusishwa nayo.

Cha kukumbuka hapo ni kwamba hata kwa Hamisa alisema ni madai tu, hadi akafikia hatua ya kuimba mistari kwenye ngoma Fresh ya Fid Q alipopewa kolabo, ambapo alikanusha uhusiano wake na Hamisa ikiwemo mtoto kuwa wake.

Kiko wapi! Kaibuka mwenyewe hivi majuzi na kumwaga mchele kwenye kuku wengi! Tutajuaje sasa… tuyaache kama yalivyo.

Na JOSEPH SHALUWA, Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364