-->

Zari Asimulia Alivyokiona Kifo cha Ivan

SIKU chache baada ya mfanyabiashara maarufu nchini Uganda, Ivan Ssemwanga ‘Ivan Don’ kuzikwa, aliyekuwa mkewe Zarina Hassan ‘Zari the Boss Lady’ ameeleza namna alivyokiona kifo cha Ivan Don.

Zari akiwa na Ivan enzi za penzi lao

Akizungumza na mtandao mmoja wa burudani, Zari alisema alipewa taarifa na madaktari mapema baada ya hali ya Ivan kubadilika.

Zari alikuwa akijibu swali aliloulizwa na mtandao huo iwapo tetesi kuwa aliyekuwa mumewe Ivan alikufa kwa sumu au lah.

“Ivan alikuwa na presha ya kupanda na hakuwahi kupima… na kama alipima hakuwahi kuichukulia serious na kuanza kutumia dawa.

“Kilichotokea ni kwamba alipata kiharusi, hapo presha nayo ikapanda… presha ikiwa juu, akapooza upande mmoja wa mwili wake ambao ulikuwa wa kushoto.

“Kiharusi kilimpiga vibaya, akapasuka mshipa kichwani ambao ulimwanga damu kwenye ubongo. Madaktari wakaniambia asilimia kubwa ya wagonjwa wa aina yake, asilimia 80 hufariki dunia mara moja.

“Asilimia 20 inayobaki, asilimia kumi huweza kufariki ndani ya mwezi mmoja na asilimia kumi nyingine; kama wakibahatika kupona huwa hawawezi kufanya chochote tena. Ni wa kuwavalisha pempasi, kuogeshwa, kulishwa na nk,” anasema Zari.

Zari anaongeza: “Baadaye wakaamua kumfanyia upasuaji lakini haikufanikiwa kwa sababu presha yake ilikuwa inapanda na kushuka kila wakati, wakamrudisha wodini kujaribu kumsaidia kwa njia nyingine.

Anasema siku mbili baadaye alipigiwa simu na daktari akamwambia aende kumuaga Ivan kwa sababu hali yake haikuwa nzuri.

Presha yake ilikuwa ikipanda hadi kufikia 220, badala ya kiwango cha kawaida cha 120 – 125, hali ambayo Zari anaielezea kuwa madaktari walimwambia haikuwa nzuri.

“Siku anafariki, nilipigiwa simu mida ya saa mbili usiku, nikaambiwa kwamba Ivan amefariki. Lakini siku moja kabla tulielezwa hilo na tulizuiwa kumtembelea wodini maana alikuwa kwenye process ya kufariki. Tukashauriwa tumwache apumzike akiwa kwenye hali ya utulivu.

“Tuliambiwa tumuage, tukafanya hivyo. Siku hiyo iliisha bila taarifa yoyote hadi siku iliyofuata saa mbili usiku. Kwahiyo siyo sumu, Ivan amekufa baada ya mshipa wa kichwani kupasuka na kusambaza damu kwenye ubongo, pamoja na kiharusi,” anasema Zari.

MAMBO YALIYOZUA GUMZO MSIBANI

Ivan Don alizikwa Jumanne wiki hii, katika makaburi ya ukoo, kijijini kwao Kayunga, nje ya jiji la Kampala, Uganda ambapo walihudhuria maelfu ya watu wakiwemo mastaa  wa Uganda na nchi jirani.

Kwa hakika maziko ya Ivan Don ambaye alikuwa kiongozi wa Kundi la Uganda Rich Gang Family, yamedhihirisha namna alivyokuwa  na utajiri wa mali na watu wenye mapenzi mema naye.

Yametokea mengi kwenye msiba huo, lakini hapa utaona  yale yaliyozua gumzo zaidi siku na wakati wa msiba wake.

DIAMOND KUTOHUDHURIA

Mpenzi wake na Zari, mwanamuziki Diamond Platnumz aliahidi kuhudhuria maziko hayo, lakini hakuweza kufanya hivyo.

Jambo hilo lilizua gumzo kubwa mitandaoni kwani wengi waliamini angefika kutokana na ahadi yake lakini hata namna alivyoonyesha utu na kujali kiasi cha kumruhusu Zari kusafiri hadi Sauzi alipokuwa akipatiwa matibabu kabla ya kifo chake.

Hata hivyo Meneja wa Diamond, Sallam SK alisema walipanga Diamond ahudhurie maziko hayo, lakini ratiba ziliingiliana.

Anasema walipanga Diamond aingie huko Alfajiri ya Jumanne, lakini ndugu wa marehemu wakaamua kusafirisha mwili usiku wa Jumatatu hivyo mipango ikavurugika.

AZIKWA NA FEDHA

Katika kile kilichoonekana kufuru, wakati mwili wa Ivan ukiwa tayari kaburini, marafiki wa marehemu Ivan, matajiri wa Uganda walianza kutupia fedha kaburini.

Ni kama vile walikuwa wakimtuza mtu, lakini ukweli ni kwamba walikuwa wakimwaga fedha kaburini, jambo ambalo lilizua maswali mengi kuliko majibu.

BIASHARA MSIBANI

Kwenye eneo la msiba kulikuwa tofauti kabisa na misiba mingine; msiba wa Ivan ulikuwa maalum na wa kistaa.

Wafanyabiashara wadogo walitumia nafasi hiyo kutengeneza fedha kwa kuuza vyakula, tisheti, kofia na vipeperushi vyenye picha na maelezo kidogo juu ya marehemu.

ZARI ATUKANWA

Wakati shughuli za msiba huo zikiendelea, Zari alikuwa akiposti picha na maelezo kwenye ukurasa wake wa Instagram ili kuwaonyesha wadau kinachoendelea, lakini wapo ambao hawakumuunga mkono na kumtolea lugha sizizo na staha.

Hata hivyo,  mwigizaji wa Bongo, Wastara Juma alijitosa kumtetea ambapo alisema wanaomsema vibaya Zari wamekosa utu.

… mimi ni mama sijawahi kusahau uchungu wa mwana na wala sijamsahau aliyenifanya niitwe mama lakini usiniulize kwanini sipo na niliyezaa naye ni mambo binafsi sana sio lazima kila mtu ajue lakini akifa nitaenda na ikibidi kulia nitalia sababu alikuwa na bado atakuwa baba wa watoto wangu…

“Lakini why why why mtu atukanweee weee asemwee kipindi kibaya cha uchungu na mawazo kama hiki? Hivi jamani mnajua kufiwa kweli wenzangu, mbona hili la Zari kutukanwa limenishinda kabisa kuvumulia. Mungu amlaze mahali pema Ivan – Amen.”

MTOTO MWINGINE WA IVAN

Baada ya kifo cha Ivan, imeelezwa kuwa mbali na watoto watatu aliozaa na Zari (Pinto, Didy na Quincy), ana mtoto mwingine mmoja wa kike.

Akifafanua hilo, Zari alisema ni kweli Ivan anaye mtoto huyo lakini siyo wa kumzaa bali alimuasili kutoka kwa kaka yake ambaye alifariki kwa kupigwa risasi na majambazi waliokuwa wakijaribu kumwibia Zari, ndipo Ivan kwa heshima akaamua kumuasili mtoto huyo kwa vile baba yake alifariki akipigania familia yake.

Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364