Brandy: N’tamkumbuka Kanumba Hadi Nakufa!
Kwenye kolamu hii leo tunaye msanii Brandy Godwin anayebamba kwenye Tamthiliya ya Kivuli katika Kituo cha Star Swahili ambaye amebananishwa ipasavyo na Mwandishi Wetu, Mayasa Mariwata na kufunguka ipasavyo kutokana na mambo mbalimbali kuhusu kazi zake na jamii inayomzunguka.
Ijumaa: Ni kitu gani kilichokusukuma kuingia kwenye sanaa ya uigizaji?
Brandy: Kiukweli napenda kuigiza sana ni kitu ambacho kipo kwenye damu. Mara ya kwanza nilipoanza kuangalia michezo ya kuigiza kipindi kile cha Kaole, nikahisi kabisa kama naweza kuigiza, mwisho wa siku nikafanya na nikaweza.
Ijumaa: Tunajua kila kona, hasa katika mambo ya maigizo kunakuwa na rushwa ya ngono, kwako ilikuwaje?
Brandy: Ishu hiyo ipo sana hata mimi nilishawahi kuombwa. Kukubali au kukataa ni matakwa ya mtu, binafsi siwezi kukubali, nataka mtu auone uwezo wangu anipe nafasi na si ngono ndiyo inipe nafasi.
Ijumaa: Ni scene gani huwa zinakupa wakati mgumu linapokuja swala la kuvaa uhusika?
Brandy: Nachukia sana scene za mapenzi kwa sababu zinaleta vishawishi, unaweza kukuta mtu unayepangiwa naye baada ya kumaliza kazi anakuganda akitaka mfanye kweli.
Mwandishi: Unapenda mwanaume wa aina gani awe mumeo?
Brandy: Anayenipenda, kunijali, kunisikiliza na kuniheshimu. Nataka kupata vitu vyote ambavyo mwanamke bora atavipata kutoka kwa mwanaume.
Ijumaa: Ni staa gani wa Bongo anayekushawishi kuwa naye kimahusiano?
Brandy: Kwa sasa sijaona, bado nipo kwenye kutafuta maisha yangu, mapenzi yapo tu!
Ijumaa: Una malengo gani katika sanaa, maana wasanii wengi wa kike hawapo ‘serious’ katika kazi hii zaidi ya kujipatia umaarufu na kupata mapedeshee, vipi wewe?
Brandy:Mimi siyo limbukeni wa pesa, kwetu mambo safi, siwi na mtu kwa sababu ya kitu bali hisia zangu pekee ndiyo zinaweza kunifanya niwe na mtu fulani, pia nina malengo makubwa kuhakikisha kipaji changu kinakuwa zaidi ya hapa.
Ijumaa: Unahisi ni kwa nini wasanii wengi wanapenda kutumia mkorogo?
Brandy: Watoto wa kike wengi wanaamini mkorogo unawaongezea urembo. Binafsi sifikirii kufanya hivyo na huu weupe alionipa Mungu, unanitosha.
Ijumaa: Akitokea mtu anataka kukupa dili ya kufanya biashara ya unga ili upate mkwanja wa haraka utakuwa tayari?
Brandy: Siwezi hata siku moja, sina uchu wa maisha mazuri kiasi hicho. Kitu kikishaitwa haramu basi jua mwisho wake huwa mbaya.
Ijumaa: Kipi kinachofanya soko la Bongo Muvi kushuka?
Brandy: Ni kutokujituma tu. Wengi wanasema kwa ajili ya kutokuwepo kwa Kanumba. Ila ukweli ni kwamba wasanii ni wavivu, hawajitumi tofauti na Kanumba ambaye usiku na mchana alikuwa akihangaika kuhakikisha anafanya ubunifu katika kazi zake. Nitamkumbuka Kanumba mpaka kifo changu!
Ijumaa:Unahisi kuwa na bifu na mtu kunaweza kukuongezea umaarufu?
Brandy: Inategemea, kuna kipindi unaweza ukawa na bifu na fulani, umaarufu ukapanda na kwa mtu mwingine, ukashuka. Wenzetu wanayajenga mabifu kwa ajili ya kazi zao kutangazwa, sisi bado hatujafika huko
Chanzo:GPL