-->

Chuchu Hans: Simtawali Ray, Nimembadilisha

STAA wa filamu za Kibongo, Chuchu Hans amefunguka kuwa staili yake ya maisha imechangia kumbadilisha tabia mpenzi wake Vincent Kigosi ‘Ray’, ambaye pia ni msanii wa filamu.

chuchu098

Chuchu aliye Miss Tanga mwaka 2005 amesema anakerwa na maneno ya watu mitandaoni kwamba anamtawala Ray, wakati ukweli ni kwamba wanaishi kwa kusikilizana.

“Watu wanaongea sana uzushi, kitu ambacho mimi kinaniumiza. Ray hakuwa hivi, mimi ndiye nimemuweka katika maisha tofauti na ushauri wangu ameufuata, sina haja ya kufafanua ila Ray wa sasa si yule wa zamani,” anasema Chuchu kwa kujiamini.

Msanii huyo anasema anajisikia vizuri kuishi maisha huru na kusikilizana na mpenzi wake, hayo mengine anawaachia ‘wanaa’ wanaohangaika kutwa, kucha na mambo ya watu.

“Mimi naona tupo vizuri, maisha yetu yanasonga.Tunashirikiana kwa kila kitu, hata kampuni yetu ya Chura, yeye ndiye amekuwa msimamizi mkuu. Anasimamia Chura na wakati huohuo RJ (ile anayoshirikiana na Johari),” anasema.

FAMILIA ZAUNGA MKONO

Aidha mwigizaji huyo alitamba kuwa uhusiano wao hauna mgogoro na kwamba hata familia zao pande zote mbili zinawaunga mkono.

“Kwetu wanamkubali na hata katika familia yao nakubalika pia. Hiyo ni kwa sababu huwa sipendi mambo ya kujibangua, ugomvi wala kujishushia heshima, naamini vitu hivyo ndivyo vimewafanya wazazi wetu watukubali,” anasema.

Chuchu na Ray ni wapenzi kwa takribani miaka miwili sasa, lakini uhusiano wao umekuwa ukinangwa na baadhi ya mashabiki wao katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

NDOA PALEPALE

Akiendelea kuzungumzia hilo Chuchu anasema: “Sitishwi na maneno ya watu. Acha waongee na najua wataongea sana, lakini mimi siwezi kuachana na Ray wangu.”

Anasema, anachojua ni kwamba riziki yake kwa nyota huyo wa filamu bado haijafa na kwamba muda ukifika watafunga ndoa yao kama walivyopanga.

“Nafarijika sana maana Ray wangu hana shida, naishi naye vizuri na kwa maelewano. Sina presha na hao wanaozungumza usiku na mchana.”

Chuchu anasema kuwa katika vitu ambavyo anajivunia sana maishani mwake ni pamoja na Ray kwani kutoka kwake, anapata kila anachotaka.

RAY ANAMDEKEZA

“Nikiwa na Ray wangu, huwa nahisi kama dunia yote ni yangu. Ray ananidekeza sana… ana mapenzi ya kweli. Ananipenda mimi na watoto wangu wawili. Amekuwa baba bora sana na hilo ndiyo linanifanya nijivunie na kuachana na maneno ya watu,” anasema Chuchu na kuongeza:

“Kufunga ndoa ni riziki na ninaamini haijafika siku yake, siku ikifika basi kila kitu kitakuwa wazi na hakuna atakayeweza kukwepa jambo hili, ila mapenzi na thamani tunayopeana ni ya mke na mume.”

Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364