-->

Eti Mimba ya Kajala Nayo Figisufigusi, Huo Sasa Utani!

kajala67

MOJA kati ya majina makubwa katika Bongo Muvi ni Kajala Masanja, ambaye kwa nyakati tofauti amebeba headlines katika vyombo vya habari.

Ni muigizaji mzuri wa kiasi chake hasa kwa levo za wacheza filamu wa nyumbani, ingawa kwa mtu mwenye mzuka wa kufika mbali, anahitaji kujinoa zaidi ili kufanikiwa kuwa zaidi ya alivyo sasa.

Kibongobongo, ni staa mkubwa, kwani ni mmoja kati ya akina dada waliocheza filamu nyingi, zilizowafikia mamilioni ya wadau nchini na hata majirani wa Afrika Mashariki na Kati kama Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na hata DRC.

Hata hivyo, kama walivyo mastaa wengi wa filamu, hasa akina dada, wanatajwa zaidi kwa mambo ya nje ya fani yao kuliko kazi zao zinavyozungumza. Sijui, lakini wadau wanasema kadiri wanavyotajwa sana kwa skendo, ndivyo soko lao linavyokuwa juu zaidi mtaani.

Kuna mtindo umeibuka ambao huenda ukazoeleka miongoni mwa mastaa wetu, hasa uhusiano wao wa kimapenzi unapohusika. Alianza Aunt Ezekiel, akafuata Wema na sasa umefika kwa Kajala (Sina kumbukumbu nzuri kama ni hao pekee niliowataja).

Ni pale wanapopata ujauzito, hawataki kumtaja mhusika. Aunt alikataa sana kumsema hadi alipojifungua na kukiri kuwa mzigo ulikuwa ni wa Mose Iyobo. Hivi sasa Wema naye yupo katika mkumbo huo, akishindwa kutoa kauli ya ni nani hasa kati ya wanaotajwa kuhusika ndiye mwenyewe.

Lakini natatizwa zaidi kwa tabia hii kuifanya Kajala, ambaye kwa muonekano, ni mkubwa kwa umri kuliko marafiki zake hao wawili. Kuna mambo mengi aliyopaswa kuyafanya kama mfano wa kupigiwa makofi, lakini amekuwa kinyume chake.

Kuna wanaume kadhaa waliokuwa karibu naye katika siku za hivi karibuni ambao wanahusishwa na ujauzito wake, wakiwemo mastaa wenzake, Diamond Platnumz na Quick Rocka, achilia mbali madai ya kuwepo kwa kigogo mmoja anayedaiwa pia kuimiliki mimba hiyo.

Nimewahi kuambiwa na mashangazi zangu kuwa mama ni mtu pekee anayemfahamu baba wa mtoto wake. Kama hivyo ndivyo, ninaamini kuwa kinachofanywa na mastaa wetu, akiwemo Kajala, siyo namna sahihi.

Kibinadamu, zinaweza kuwepo hisia kuwa wasichana hawa wanashindwa kumtaja mhusika kwa vile wanakuwa wamewapa mimba hiyo watu wengi, ambao wanategemea ndiyo wawatunze kwa mahitaji yao ya kila siku.

Anajua, akimtaja mtu kuwa ndiye mhusika, atakosa huduma kutoka kwa mpenzi X, Y, au Z. Kama hivi ndivyo, basi ni ishara ya wazi kuwa mastaa wetu siyo watu wa kuaminika katika maisha yao ya kimapenzi.

Kwa sababu tunawajua hata waigizaji na wasanii wengine wenye majina Ulaya na Marekani, wana-date na watu wengi, lakini siyo kwa wakati mmoja. Mtu mmoja kwa wakati wake, ndiyo maana hata ikitokea wamenasa, huweka wazi kuwa ujauzito huu ni wa mtu f’ lani!

Jambo hili lilipaswa kufanywa na Kajala pia, siyo kwa sababu nyingine yoyote zaidi ya kulinda hadhi ya jina lake. Ni kweli yeye anamfahamu mhusika, sasa kwa nini hamtaji ili mashabiki wake watambue, waachane na hisia hizi?

Tunapata mifano mingi ya wanaume kubambikwa watoto kwa staili hii. Msichana anakuwa na wanaume zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja na kila mtu anaambiwa ni mali yake. Watu wanahudumia wakijua watoto wao, mwisho wa siku inabaki kuwa aibu kwa mwanamke.

Mastaa kama Kajala, Wema na wenzao, wanatakiwa kuwa mfano mzuri wa kuwataja wenye ujauzito wao, ili jamii yote ijue, kuepuka kesho na keshokutwa anapojitokeza mtu mwingine na kuanza kuleta figisufigisu.

Chanzo: GPL

 

Comments

comments

Post Tagged with

Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364