-->

JPM Atema Cheche Waliofungwa kwa Dawa za Kulevya

Serikali imesema kamwe haitawatetea Watanzania wanaotumikia vifungo katika magereza mbalimbali nje ya nchi kutokana na kujihusisha na dawa za kulevya.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Bw.Rogers William Sianga kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Pia imesema itakachokifanya ni kuzishauri serikali za nchi husika kutekeleza hukumu dhidi ya Watanzania hao kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi husika.

Msimamo huo wa serikali umetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam hii leo, katika hafla ya kuwaapisha viongozi aliowateuwa hivi karibuni kati yao wakiwemo Kamishna wa Uhamiaji, Mkuu wa Tume ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya pamoja na mabalozi.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, tatizo la dawa za kulevya ni vita inayopaswa kupiganwa na kila mmoja na kwamba ni mujibu kwa vijana nchini kuacha kujihusisha na uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya kwani ni hatari kwa afya zao na usalama wa nchi.

Mhe. Rais Magufuli amewapongeza viongozi wote wa mikoa walioanza kukamata watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya na amewaomba Watanzania wote waunge mkono juhudi za kukabiliana na wanaofanya biashara na kutumia dawa za kulevya ambazo zinazidi kuangamiza nguvukazi ya Taifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli

“Niwaombe ndugu zangu tuungane katika vita hii dhidi ya dawa za kulevya, waandishi wa habari na wana mitandao tuweke mbele Utanzania wetu, akitokea mtu anapambana na dawa za kulevya tumuunge mkono badala ya kumchafua.

“Vita hii ni kubwa hatuwezi kwenda nayo kwa mzaha na Serikali itahakikisha inasimamia sheria namba 5 ya mwaka 2015 iliyohusu kuzuia na kupambana na dawa za kulevya ambayo ilitungwa na Bunge la 10 lililoongozwa na Spika Anna Makinda na sheria hiyo ikatiwa saini na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, nawapongeza sana kwa kutunga sheria hii.” Amesisitiza Mhe. Rais Magufuli

Pia, Mhe. Dkt. Magufuli amesema takwimu zinaonesha kuna watanzania 1,007 wamekamatwa na kufungwa gerezani katika nchi mbalimbali baada ya kupatikana na makosa ya kujihusisha na dawa za kulevya, na amemuagiza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mabalozi wote wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi hizo kutojihusisha kuwatetea waliofungwa kwa makosa hayo na badala yake waache sheria za nchi husika zichukue mkondo wake.

Viongozi walioapishwa leo Ikulu Jijini Dar es Salaam wakila kiapo cha Maadili katika utumishu wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili katika Sekretariat ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Mhe. Jaji Harold Nsekela 

Katika hotuba yake iliyoendana na maagizo kwa vyombo vya ulinzi na usalama, Rais Magufuli amesema amepongeza hatua zinazochukuliwa na baadhi ya viongozi nchini katika kupambana na dawa za kulevya na kwamba katika vita hiyo hakuna wa kumuonea haya.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri na Makatibu Wakuu baada ya kuwaapisha Mabalozi na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Ikulu Jijini Dar es Salaam.

EATV.TV

 

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364