Le Mutuz Ajitapa Kutoka Kimapenzi na Amanda
NISHAI! William Malecela ‘Le Mutuz’ juzikati aliumbuka baada ya kuposti ujumbe kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram, akijitapa kwamba amewahi kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwigizaji maarufu Bongo, Tamrina Posh ‘Amanda’, jambo lililosababisha wachangiaji wamshukie vikali kwa maneno ya kuudhi.
Katika ujumbe wake, Le Mutuz ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu wa Saba wa Tanzania na mwanasiasa mkongwe, John Samwel Malecela, aliandika kwamba baada ya kurejea kutoka ng’ambo alikoenda kimasomo miaka mitano iliyopita, Amanda ndiye aliyekuwa mwanamke wake wa kwanza kutoka naye kimapenzi.
Baada ya kuposti ujumbe huo, wachangiaji walimshukia, wengi wakimlaumu kwa kukosa busara kwani kama walikuwa wapenzi, hayo ni masuala yao binafsi na yalishapita hivyo hakuna sababu yoyote ya kujisifia wakati walishaachana kitambo. Hali hiyo ilisababisha Le Mutuz afute haraka ujumbe huo ambao hata hivyo, tayari ulishaonwa na watu wengi ambao waliendelea kumponda.
Baada ya kuunasa ‘ubuyu’ huo, Risasi Jumamosi lilimtafuta Le Mutuz kupitia namba yake ya simu ya kiganjani ili kujua sababu za yeye kuposti ujumbe lakini mpaka gazeti hili linakwenda mitamboni, simu yake haikuwa ikipatikana hewani.
Kwa upande wa Amanda alipotafutwa, alisema:
“Hayo mambo yalishapita, ilitokea ikapita. Sasa hivi mimi na yeye ni marafi ki tu, mimi nina mtu wangu na yeye ana maisha yake kwa hiyo sioni kama ni busara kuyazungumzia,” alisema Amanda.
Chanzo: GPL