Pichaz: Jinsi Wachimbaji 15 Walivyookolewa Baada ya Kufukiwa kwa Siku 4 Kwenye Kifusi Mgodini Geita
Wakiwa wameloa mwili mzima na tope la udongo mwekundu wa mgodini uliokuwa umezifunika nguo zao, wachimbaji hawa 15, hawakuamini macho yao baada ya kuliona tena jua kwa mara ya kwanza, kufuatia kuwa chini ya ardhi, kwa siku nne mfululizo.
Miili yao haikuwa na nguvu, tumboni hakukuwa na kitu na njaa ya siku nne ilikuwa imewatafuna vilivyo kiasi cha kushindwa kusimama kwa miguu yao miwili baada ya kuokolewa.
Kwa wachimbaji hawa wa mgodi wa RZ uliopo mkoani Geita, nafasi ya pili ya kuishi waliyopewa, itakuwa ni kumbukumbu ambayo hawataisahau kamwe katika maisha yao.
Kutenganishwa na mazingira ya kawaida ya dunia na kuwa chini ya kifusi cha mgodi ambako harufu ya kifo ilianza kuwa dhahiri kwenye pua zao, ni mkasa utakaobaki daima vichwani mwao na utakuwa kama mkanda wa video utakaojirudia kucheza vichwani mwao kwa miaka mingi.
Baada ya zoezi la uokoaji, wachimbaji wote 15 waliokolewa Jumapili hii katika mgodi huo wa dhahabu uliopo Nyarugusu mkoani Geita. Zoezi halikuwa rahisi katu na lilidumu kwa siku tatu.
Kwa wananchi wengi waliokuwa wamekusanyika jirani na mgodi huo, tukio hilo lilikuwa kama filamu wakati wakiwashuhudia wachimbaji hao wakitolewa mmoja baada ya mwingine.
Baadhi yao, wakiongea kwa tabu walieleza kuwa, kukaa kwa siku nne kwenye kifusi hicho kuliwakatisha tamaa na kuzishuhudia siku zao za kuishi duniani zikikiyoyoma kila mshale wa saa ulivyokuwa ukitembea.
Na sasa wakiendelea kupatiwa matibabu kwenye hospitali ya mkoani Geita, baada ya kupewa huduma ya kwanza punde walipookolewa, wanaendelea kukusanya nguvu, na pale zitakapowaijia, bila shaka watahitaji muda wa kutafakari mustakabali wao baada ya kukikwepa kifo, katika shimo lenye udongo uso na huruma.
Na kwa miaka mingi, mioyo yao itabeba shukrani za dhati kwa waokoaji waliokesha kuchimba shimo walimokuwa wamefukiwa ili kuutetea uhai wao uliokuwa nchani kutoweka.
Picha: Maduka Online Blog
Bongo5