Rose Muhando Afungukia Kimya Chake na Tuhuma ya Kutumia ‘Unga’
Muimbaji mashughuli wa nyimbo za injili hapa nchini,Rose Muhando amevunja ukimya na kufuka juu ya ukimya wake na tuhuma za kutumia madawa ya kulevya ‘Unga’.
Akiongea na gazeti la mwanaspoti hivi karibuni, Rose anasema, amekuwa kimya kwa sababu mbalimbali lakini anawaambia mashabiki wake yupo na anafanya maandalizi mengine: “Nipo hata hivyo kuna kazi nyingine nimeandaa ipo kwa Alex Msama bado haijatoka kutokana na mambo mbalimbali, ingawa naandaa kazi nyingine ninayotegemea kuikamilisha mwezi wa tatu mwakani tutakapojaaliwa. Nimeshaanza kuandaa baadhi ya nyimbo na nyingine naendelea kutunga, unajua kazi hizi huwa nasikiliza sauti ya Mungu aniambie niimbe nini.”
“Pia, nimekuwa nafanya huduma ya kuimba katika mikutano tofauti ndani na nje ya nchi kama hivi jana umenikuta natoka kijiji cha jirani kuimba na wiki iliyopita, nilikuwa Kenya ambako nilifanya huduma, Kisumu na Mombasa, nimeamua kufanya hivyo kwa sababu zangu,”anasema Rose.
Kuhusu tuhuma ya madawa ya kulenya, Rose alisema “Situmii madawa na sitatumia, kama waliona ndiyo skendo itakayonimaliza wameshindwa, wanaofanya hivyo ni watu wanaotaka kunimaliza walitaka nifanye kazi zao, nikakataa.”
“Sijajiingiza na mambo hayo na wanavyozungumza nasikitika kwa sababu wanaiumiza familia yangu kisaikolojia, mimi ni mama wa watoto watatu na nina ndugu zangu, naambiwa mambo yote hayo kwa sababu sina mtu wa kunitetea,”anasema Rose.