Spika Awakumbusha Wapinzani Kuwa Nao Wana Mawaziri Wakuu Wastaafu
Wakati wa mjadala huo, Spika wa Bunge, Job Ndugai amewakumbusha wabunge wa upinzani wanaotaka marais wastaafu washtakiwe kuhusu sakata la mchanga wa madini, wakumbuke wanao mawaziri wakuu wastaafu wawili ambao watahusika pia.
Ndugai amesema hayo leo (Jumanne) bungeni baada ya mchango wa Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali kusema haiwezekani mawaziri na watendaji wengine wa Serikali wakafanikisha mikataba mibovu ya madini bila ridhaa ya Rais.
“Haiwezekani mzee wangu (Andrew) Chenge na (Nazir) Karamagi walipitisha mikataba hiyo bila Rais aliyekuwapo kufahamu. Kinga ya Rais kushtakiwa iondolewe ili wahojiwe,” amesema Lijualikali.
Baada ya hoja hiyo ya Lijualikali inayofanana na ya Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Ndugai aliwakumbusha juu ya mawaziri wastaafu walionao kwenye chama chao.
“Mabadiliko mnayoyataka yakipitishwa na viongozi mlionao wakikamatwa msije mkalalamika tena,” amesema Ndugai.
Wakati huo huo, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa amesema haipendezi kuwaita wawekezaji wa madini wezi kwani waliwekeza kwa kufuata sheria na taratibu zote.
Amesema mara zote Rais wa CCM hukabidhiwa ilani ya chama ambayo ina sera kwa ajili ya utekelezaji wa masuala mbalimbali yakiwamo madini. “Mtuambie (CCM) Sera yenu ya madini ni ipi?” amesema Msigwa.