-->

Hawa Ndiyo Wanawake Waliong’ara 2016

Tunaendelea na wanawake waliong’ara mwaka 2016 kwa kutoa maelezo kigo kuhusu walichofanya.

Khadija Mwanamboka

Wengi wanamfahamu Khadija Mwanamboka kutokana na tasnia ya mitindo. Alikuwa miongoni mwa wabunifu waliohamasisha Watanzania kuvaa mavazi yanayotengenezwa na wabunifu wa hapa nchini. Mwaka 2016, aligeukia upande mwingine na kujihusisha zaidi na biashara ya chakula.

Kupitia chapa yake ya Vitu vya Khadija (VVK), anatengeneza bidhaa mbalimbali kama kashata, ubuyu, mbilimbi, chachandu na kuzifungasha kisasa.

Dk Agnes Kijazi

Jina la Kijazi liko katika uongozi wa juu na Dk Agnes Kijazi ni mmoja wa wenye jina hilo aliye na nafasi kubwa. Ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA). Mama huyu ameiongoza vyema taasisi hiyo inayotoa taaridfa za ubashiri wa hali ya hewa ambazo hutumiwa na wataalamu mbalimbali kupanga mipango yao kama ilivyo kwa wananchi wengine ambao huzitumia kwa kilimo na shughuli nyingine.

Amefanikiwa kurudisha imani ya wananchi kwa taasisi hiyo ambayo awali ilikuwa haiaminiki.

Dk Mwele Malecela

Dk Mwele Malecela amemaliza kwa staili ya aina yake; ametoa taarifa ya matokeo ya utafiti kuhusu kuwepo kwa wagonjwa wa ugonjwa hatari wa zika; na pili amevuliwa ukurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR). Hayo yametokea zaidi ya mwaka mmoja tangu ajitose bila ya mafanikio kuwania urais kwa tiketi ya CCM.

Ni bingwa wa magonjwa yanayoenezwa na mbu wa aina tofauti, hasa mabusha na matende na ameendesha kampeni nyingi kupambana na magonjwa hayo na pia kufanya tafiti ambazo mojawapo imeamua hatima yake.

Sarah Raqey

Sekta ya ujasiriamali imeendelea kupokea wanawake wengi wanaojihusisha na biashara ya vyakula, Sarah Raqey akiwa mmoja wao.

Dada huyu amejijengea umaarufu mkubwa kwa kutoa huduma hiyo kisasa, hasa kwenye mikutano, hafla na vikao vikubwa vya kampuni na taasisi mbalimbali.

Rita Paulsen

Anaitwa Rita Paulsen, lakini wengi tunamfahamu kama Madam Rita, yule muandaaji wa shindano la kuibua vipaji la Bongo Star Search.

Mwaka huu ameanzisha kipindi cha runinga kinachogusa maisha ya vijana katika nyanja mbalimbali.

Rest Bura Kweka

Unapowataja wanawake ambao wamejitoa kindaki kwenye ujasiriamali Rest Bura Kweka hakosekani kwenye orodha hiyo. Mwanadada huyu amejikita kwenye upishi wa vyakula anavyovisambaza sehemu mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Upishi wake wa samaki, ndizi, chips na mishkaki umelenga kuwanasa wafanyakazi, hasa vijana ambao ni makapera.

Jenista Mhagama

Kati ya wanawake wanaozidi kubobea kwenye uongozi wa ngazi ya uwaziri, ni pamoja na Jenista Mhagama. Yumo tena kwenye Baraza la Mawaziri la Serikali ya Awamu ya Tano.

Katika nafasi yake ya Waziri akishughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, ameonyesha uchapakazi mzuri. Ni miongoni mwa mawaziri ambao mwaka 2016 wametumia muda mwingi kuwafikia Watanzania na kutatua changamoto zao kuliko kukaa ofisini.

Magdalena Sakaya

Ni miongoni mwa wanasiasa wanawake ambao majina yao mara kadhaa yamepamba vyombo vya habari. Magdalena Sakaya ni naibu katibu mkuu wa CUF lakini alitangazwa kusimamishwa baada ya kuhusika kwenye mgogoro wa chama hicho.

Bado anaendelea kupambana akimuunga mkono Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye amevuliwa uenyekiti wa CUF lakini anatambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.

Sweet Lorah

Ukizungumzia wanawake waliosimama kindakindaki kwenye biashara, Sweet Lorah ni mmoja wao. Amejikita zaidi kwenye biashara ya nguo za kisasa, hasa za watoto.

Evelyn Rugemalira

Kupitia chapa yake ya Eve Collections, Evelyn ameingia kwenye orodha ya wabunifu wa mavazi ya wanawake wanaofanya vizuri nchini.

Tofauti na wengi ambao licha ya vipaji walivyonavyo wameingia kwenye ubunifu kwa lengo la kutafuta fedha, Evelyn Rugemalira alijikuta katika tasnia hiyo wakati akisaka nguo zinazoendana na mwili wake.

Kiki Zimba

Kiki Zimba anamiliki lebo ya mavazi ya Kiki’s Fashion na amejijengea umaarufu mkubwa kutokana na uwezo wake wa kubuni na kutengeneza mavazi ya kisasa kwa kutumia malighafi za kiafrika, kama khanga na vitenge.

Ameendelea kuwavalisha watu maarufu na nguo zake kupamba majukwaa ya maonyesho mbalimbali ya mavazi nchini.

Aneth Isaya

Ni mwanadada ambaye alizaliwa akiwa mzima wa afya, lakini baadaye akapata tatizo la kutokusikia.

Aliendelea na masomo na baadaye alifanikiwa kupata shahada yake ya kwanza, lakini alijitahidi kutafuta kazi bila mafanikio. Kila alipopata nafasi alikataliwa kutokana na ulemavu huo.Baadaye aliamua kuanzisha Taasisi ya Furaha ya Wanawake Wajasirialiali kwa Viziwi Tanzania (Fuwavita) akiwa kama mkurugenzi mtendaji.

Baadaye aliamua kujikita kwenye ujasiriamali na kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwemo peanut butter na mango pickle.

Lady Jaydee

Mwaka 2016 umekuwa ni wa kipekee kwa mwimbaji huyu mkongwe wa bongo fleva baada ya kupambana na mambo mengi mazito, na kufanikiwa kurejea kileleni kwa kishindo.

Alivunja ukimya wa muda mrefu baada ya kurudi na wimbo wa “Ndi Ndi Ndi” ulioonekana kupokelewa vizuri na mashabiki.

Alifanya onyesho la aina yake wakati wa uzinduzi, akijaza ukumbi wa Mlimani City. Amenyakua tuzo ya Mwanamuziki Bora wa Kike wa EATV.

Jaydee, ambaye jina lake halisi ni Judith Wambura, anafunga mwaka kwa kutoa wimbo mpya alioshirikiana na mpenzi wake mpya raia wa Nigeria aitwaye Spicymuzik.

Maza Sinare ‘Maznat’

Huyu ni mjasiriamali ambaye amejikita kwenye huduma zinazowahusu wanawake. Ana saluni maarufu jijini Dar es Salaam ya Maznat Saloon. Kama ilivyo ada mwaka 2016 ameendelea kufanya vizuri kwenye upambaji wa mabibi harusi.

Maznat pia ama sehemu yake ya kushona nguo za maharusi inayofahamika kama Maznat Tailor. Pia ana duka la maua ya maharusi.

Hamisa Mobetto

Ni miongoni mwa wanamitindo wanaofanya vizuri nchini. Mrembo huyu ambaye ni mama wa mtoto mmoja amefanikiwa kuvuka mipaka na mwaka huu amepata tuzo ya Best Dressed Lady iliyotolewa Afrika Kusini.

Hivi karibuni, Hamisa pia alinyakua tuzo ya Mwanamitindo Bora wa Instagram. Amekuwa akitumika kutangaza kazi za wabunifu maarufu nchini.

Kylin

Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi, ambaye alikuwa Miss Tanzania 2000 amefanikiwa kufanya mengi katika jamii ikiwa ni pamoja na kuanzisha mfuko maalum wa kusaidia watoto wasio na uwezo.

Septemba mwaka huu alizindua duka lake jipya la Amorette lililopo Sea Cliff, Masaki jijini Dar es salaam. Linauza samani za ndani chapa ya Molocaho.

Duka hilo linauza vitu vya aina tofauti kama makochi, viti, vitanda na meza na anatarajia kuongeza samani za jikoni.

Upendo Mwalongo

Ameingia kwenye orodha hii baada ya kufanya vizuri mwaka huu upande wa ujasiriamali. Kupitia lebo yake ya Openkitchen amepata mialiko ya kutoa huduma ya chakula kwenye hafla na sherehe mbalimbali.

Amejikita pia kwenye kupika na kuuza vyakula. Umahiri wake katika upishi umekuwa chachu ya kujitengenezea umaarufu na kupata wateja wengi jijini Dar es Salaam.

Jennifer Shigoli

Alipeperusha vyema bendera ya Tanzania na kunyakua tuzo katika tamasha la Mjasiriamali Bora wa Afrika lililofanyika Marekani.

Shigoli alitwaa tuzo hiyo katika kipengele cha elimu ya pedi zinazoweza kutumika tena (Reusable Sanitary Pads) na kunyakua dola 150,000 za Kimarekani.

Tuzo hizo ziliandaliwa kwa ushirikiano kati ya benki ya BMCE na African Entrepreneurship Award.

Seven Mosha

Huyu ni meneja Ali Kiba. Licha ya kuwa anayoifanya haipi nafasi ya kuonekana kama ilivyo kwa msanii wake, Seven ameonyesha umuhimu wake kama meneja kwa Ali Kiba.

Kwa mwaka 2016, Seven amefanya kazi kubwa ya kumtangaza Ali Kiba na kudhihirisha hata wanawake wanaweza. Pia anamsimamia Lady Jay dee.

Johanna Matthysen

Kwenye mitandao ya kijamii anafahamika kama Directorjoan. anatumia fursa ya mitandao ya kijamii kutangaza shughuli zao za ujasiriamali. NI mmoja wa wajasiriamali waliotumia uwanja huo kukuza biashara zao.

Makala Kutoka:  Gazeti la Mwananchi Mtandaoni

 

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364