-->

Yaliyobamba, kutikisa 2017

MASHABIKI wa burudani na sanaa nchini wanahesabu siku tu kabla ya kuuaga rasmi Mwaka 2017 na kuukaribisha Mwaka Mpya wa 2018.

Hesabu zinaonyesha zimesalia siku 9 tu ambazo ni sawa na saa 216 kabla mwaka haujakatika.

Lakini mwaka ukiwa unaelekea ukingoni, kuna mambo mengi yaliyojiri yatakayokumbukwa ambayo baadhi yalikuwa ya furaha, mengine ya huzuni na yalikuwapo ya kustaajabisha pia.

Mwanaspoti linakuletea kwa muktasari baadhi ya matukio yaliyobamba na kutikisa ndani ya Mwaka 2017 bila kujali ni ya aina gani.

MASTAA NA UZAZI

Kwa hakika 2017 ulikuwa mwaka wa uzazi kutokana na wasanii wengi hasa wa kike kuamua kujiachia na kujifungua watoto kana kwamba wapo kwenye mashindano.

Pazia lilifunguliwa na mshiriki wa Shindano la Bongo Star Search (BSS), Menina, aliyejifungua mtoto wa kiume Februari 9 kabla ya kufuatiwa na wakali wengine kibao.

Mwanamitindo Hamisa Mobeto naye alijifungua mtoto wa kiume, Esha Buheti anayekimbiza katika Bongo Movie hakuwa nyuma alijifungua mtoto wa kike.

Wengine waliofyatua watoto ni Linah Sanga, Faiza Ally, Chuchu Hans, Miss Tanzania 2001 Happiness Magese aliyezaa mtoto wa kiume baada ya kilio cha miaka mingi akipigana vita kali na ugonjwa wa endometriosis.

MISIBA KILA KONA

Kila anayezaliwa, lazima aonje mauti. Katika sanaa pia kulikuwa na huzuni kutokana na vifo kadhaa vilivyojitokeza ndani ya 2017.

Mkali wa Mchiriku, Mfaume Selemani ‘Dogo Mfaume’, alianza kuwatia simanzi mashabiki kwa kifo chake cha ghafla.

Wakati mashabiki wakitafakari msiba huo, gwiji wa muziki wa dansi nchini, aliyekuwa Msondo Ngoma, Shaaban Dede naye aliaga dunia baada ya kuteseka hospitalini kwa muda mfupi.

Wakali wengine walioaga dunia ndani ya mwaka huu ni Halila Tongolanga aliyetesa na wimbo ‘Kila Munu Ave na Kwao”, mwigizaji Kijakazi Pazi Shaaban ‘ Zamzam ‘ aliyewahi kutamba Kidedea naye alifariki dunia. Kifupi haukuwa mwaka mzuri kwa upande wa sanaa.

NDOA ZILINOGA

2017 ulinoga kwa namna wasanii walivyochuana kuziaga kambi zao za ukapera kwa kuingia kwenye ndoa.

Kuanzia kwa Profesa Jay ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Mikumi, Flora Mbasha mkali wa muziki wa Injili, Joti anayetamba kwenye vichekesho, mpaka Dogo Janja na Irene Uwoya ni kuonyesha namna gani huu ulikuwa mwaka wa aina yake.

Sijamsahau Shilole na Uchebe walioamua kufunga ndoa kimya kimya japo waliitangaza ingefanyika Desemba 20.

Ndoa iliyokuwa gumzo ni ile ya Joti, pia ile ya Dogo Janja mpaka leo kuna baadhi ya mashabiki bado hawaamini kama ilifanyika ama ilikuwa sehemu ya kazi zao za sanaa.

MZEE YUSUF ASHTUSHA

Kama kuna tukio lililowashtukiza mashabiki wa sanaa hasa wale wa muziki wa taarab basi ni kitendo cha Mfalme Mzee Yusuf kutangaza kuachana na kazi hiyo.

Mzee alitangaza ameacha muziki ile ajikite katika masuala ya kumtumikia Mwenyezi Mungu na Mtume Muhammad SAW

Baada ya kuacha muziki mwimbaji huyo alienda kuhiji Makka kwa nia ya kutubu kwa Mola wale na kujikita katika kutoa mawaidha ya dini yake ya Kiislamu.

SAIDA KAROLI AIBUKA

Baada ya ukimya wa miaka mingi hatimaye mwaka 2017 ulishuhudia Saida Karoli akiibuka upya na kufanya yake akiwarejeshea imani mashabiki wake kuwa bado wamo.

Ziara yake ya Miaka 15 tangu afanye sanaa, ilimfanya Saida kurejesha heshima yake ya enzi za Chambua Kama Karanga na Mapenzi Kizunguzungu, hata hivyo ilikuwa kwa muda tu na baadaye kuwa kimya.

Hakutofautiana sana na Darasa aliyesumbua na kazi yake ya Maisha na Muziki uliofunika ndani na nje ya Tanzania, hata hivyo baada ya hapo mambo yamepoaaa.

PENZI LA WOLPER, HARMONIZE

Mapenzi yao yalianza kama utani mwaka jana kiasi cha watu kudhani ni kiki tu, lakini baadaye ikabainika ni kweli na wawili hao kujiachia kwa raha zao.

Hata hivyo kama wasemavyo wahenga, ngoma ivumavyo haikeshi, penzi la wawili hao liliishia njiani na kila mmoja kashika lake.

VANESSA NA JUX NAKO

Juni mwaka huu, mkali wa muziki wa kizazi kipya, Vanessa Mdee alithibitisha kutemana na mpenzi wake, Jux, kitu kilichowashtua mashabiki wao.

Hii ni kwa sababu hakukuwa na dalili za ‘kapo’ hiyo kutibuana, lakini ikawa hivyo kabla ya wawili hao kuamua kurejesha majeshi nyuma na kurudiana hivi karibuni.

WALILALA SELO

Wasanii kadhaa walikumbana na vimbwanga ikiwamo baadhi yao kulala selo kama ilivyomkuta ‘Nay wa Mitego’ kisa wimbo wake wa ‘Wapo’ uliotafsiriwa ulilenga kuwakashfu viongozi wa kiserikali, baadhi ya watu wenye majina makubwa kwenye jamii.

Orodha hiyo pia ina kina Wema Sepetu, ‘Masogange’ (kesi zao zinaendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu), Winfrida Josephate ‘Recho’, Tunda Sebastian, Vanessa Mdee ‘V-Money’, Khaleed Mohamed ‘TID’, Petit Man, Babuu wa Kitaa nao walipa kuionja selo.

Baadhi yao waliingia matatani kwa tuhuma za dawa za kulevya.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaama, Paul Makonda alitoa orodha ya wasanii waliokuwa wakidaiwa kujihusisha na matumizi pamoja na biashara ya dawa za kulevya.

Ni kitu ambacho kilishtua sana kwani hakuna aliyetengemea na ni kitu ambacho hakikuwahi kufanyika hapo awali.

Ndipo baadhi yao wakajikuta msambweni akiwamo TID, Nyandu Tozi, Babu wa Kitaa, Romy Jones, Tunda, Mr. Blue, Vanessa Mdee, Wema Sepetu na wengine.

DIAMOND AJIANIKA

Tangu Diamond alipomshirikisha Hamisa Mobetto katika video ya ngoma yake ‘Salome’ zilianza kuenea tetesi kwamba mkali huyo keshampitia dada huyo, lakini akapotezea.

Hamisa alipoibuka na ujauzito vidole vilielekezwa kwa Diamond, lakini mwenyewe akauchuna kabla ya siku ya mwisho baada ya kuzaliwa kwa mtoto akaibuka kujianika.

Diamond alijianika Septemba 19 katika mahojiano na kituo cha redio kuwa ni kweli kazaa na Hamisa na kuweka bayana mambo kibao .

Kilichofanya stori hii kuwa kubwa zaidi ni pale Diamond aliposema baada ya Hamisa kubeba ujauzito alimnunulia gari aina ya Rav4 na kutoa sh. milioni. 7 na laki 5 ili kumpeleka hospital ya Private kwa ajili ya kujifungua.

Hata hivyo siku chache baadaye msanii huyo aliburuzwa mahakamani na Hamisa kisa matunzo ya Abdul Junior.

BABU SEYA, PAPII KOCHA WAACHIWA

Kama kuna tukio lililobamba 2017 basi ni hili lililotokea Desemba 9, ambapo ilikuwa siku ya Uhuru wa Tanganyika iliposhuhudiwa Rais John Magufuli akiwasaprize raia wake.

Rais Magufuli alitangaza kuwasamehe Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye Papii Kocha waliokuwa wakitumikia kifungo cha maisha kwa kosa la unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto.

Wanamuziki hao walihukumiwa kifungo hicho mwaka 2004 na walishakata rufaa zaidi ya mara mbili na zote ziligonga ukuta kabla ya Rais Magufuli kuwatoa kiulaini.

ROMA HANA HAMU

Usiku wa Aprili 6 kulianza kusambaa kwa taarifa za msanii Roma, Moni na Prodyuza Bin Laden kutekwa na watu wasiojulikana wakiwa katika Studio za Tongwe Records.

Tukio hili liligonga vilivyo vichwa vya habari kwa vyombo vya habari kwa hapa Tanzania na nje ya nchi ukiachilia mbali harakati mbali mbali zilizokuwa zikiendelea katika mitandao ya kijamii ‘FreeRoma’.

Kwa uzito wake haikuwa ajabu kusikia/kuona wabunge kadhaa na mawaziri wakisimama bungeni na kulizungumzia.

Baada ya hayo yote hatimaye Roma na wenzake walipatikana wakiwa hai ingawa walikuwa na majeraha mbali mbali katika miili yao. Roma akaja akatoa ngoma yake ya kwanza ‘Zimbabwe’ tangu kutokea kwa tukio hilo na maisha mengine ya kimuziki kuendelea.

WEMA NA SIASA

Ndani ya mwaka huu gumzo ilikuwa Wema kuondoka CCM na kwenda Chadema kabla ya kutangaza tena kurudi CCM.

Ipo hivi mwanadada huyo Februari 24 alijiunga na Chadema, huku ikielezwa ni hasira za misukosuko ya ishu yake ya kesi inayomkabili, japo alikanusha.

Hata hivyo Desemba Mosi alitangaza kurudi CCM na kuipiga chini Chadema hivyo kuonekana hana msimamo.

DIAMOND, KIBA NAO

Ule mchuano baina ya Diamond na Ali Kiba uliendelea kuwagawa mashabiki na hasa baada ya wawili hao kuachia ngoma zilizosumbua sana kwa wakati mmoja.

Kiba aliachia Seduce Me, kabla ya siku chache WCB chini ya Diamond kuachia Zilipendwa na kufanya yaibuke malumbano mitandaoni kwa mashabiki wa nyota hao.

Hata hivyo baadaye upepo ulitulia, lakini Diamond na crew yake wakajikuta wakipokea notisi, ya kutakiwa kulipa Sh 300 milioni kwa Msondo Ngoma Band kwa kutumia kazi zao bila ridhaa yao.

Wakongwe hao wa muziki walilalamikia kitendio cha WCB kutumia ala yao iliyopo kwenye wimbo wao wa Ajali bila kuomba ridhaa, hata hivyo mpaka sasa ishu ipo kimya tu.

By RHOBI CHACHA, Mwanaspoti

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364