-->

Eshe Buheti Miaka 13 ya Ndoa, Siyo Mchezo

MIONGONI mwa wasanii nyota wa filamu za Kibongo ni pamoja na Eshe Buhet. Uwezo wake wa kuigiza ndiyo uliomfikisha alipo leo hii, msanii huyu ambaye mchango wa mkongwe, Issa Mussa ‘Cloud 112’ ni mkubwa maana ndiye prodyuza wa kwanza kumchezesha na kumtambulisha.

ESHA23

Eshe ambaye ni mzaliwa wa Tanga na kulelewa jijini humo alikuja jijini Dar es Salaam kama mfanyabiashara, ndipo wasanii wakongwe walipoona kipaji chake na kumtumia, bahati nzuri hakuwaangusha, akazidi kuchanua.

Uwezo wa Eshe unajidhihirisha zaidi katika Filamu ya ‘Mimi na Mungu Wangu’  ambayo ilimfanya aweze kuondoka na Tuzo ya Msanii Bora wa Kike, mwaka jana zilizotolewa na ZIFF katika Tamasha la Kimataifa la Filamu la Nchi za Jahazi ‘ZIFF’ lililofanyika mjini Unguja, Zanzibar.

Polisi wa Swaggaz alikutana na Eshe na kuzungumza naye mambo mbalimbali kuhusu maisha yake binafsi na ndani ya filamu, hasa kuhusiana na fununu za ndoa yake kuvunjika.

Msanii huyu tofauti na wengine wengi ambao ndoa zao huvunjika ndani ya muda mfupi, yupo kwenye ndoa kwa miaka 13 sasa huku akidai kuwa  jinamizi la kuachana likifukuta mitaani, wakati ndani ya ndoa yake kukiwa na amani tele.

DILI JIPYA

Anasema, ushindi wa tuzo ya ZIFF umempa dili la kucheza tamthilia nchini Kenya kwa malipo mazuri.

“Nashukuru sana kupata tuzo ile. Kwa ushindi ule nimefanikiwa kupata mkataba nchini Kenya ambako kuna tamthilia nashiriki. Inaitwa Kashfa, imechezwa zaidi na Wakenya, lakini kwa upande wa Tanzania, tupo mimi na Yusuph Mlela.

“Hao jamaa wa hiyo tamthilia walinikubali baada ya kuniona ZIFF nikichukua tuzo na kazi nilizofanya. Najua huo ni mwanzo, milango itazidi kufunguka zaidi kimataifa,” anasema.

NI KWELI AMEACHIKA?

Ipo minong’ono kuwa ndoa yake imevunjika, akizungumzia hilo anasema, bado yupo kwenye ndoa na anaishi kwa amani na mume wake ingawa watu wanasambaza maneno kuwa wametengana.

“Niliolewa tangu mwaka 2008, nimefanikiwa kupata mtoto mmoja wa kike na ninaishi kwa amani na upendo na mume wangu. Nashangaa ambao wanasema nimeachika, mimi nipo katika ndoa yangu na sitarajii kuachika kwani najua kuchukua majukumu yangu kama mama.

“Nawajua Wabongo, wameanzisha maneno hayo ili nimuonyeshe mume wangu kwenye mitandao, katu sitafanya hivyo. Sifanyi maisha kwa ajili ya watu, naishi maisha yangu halisi.

“Wapo mastaa wenye tabia ya kuwaonyesha wapenzi au waume zao kwenye mitandao, ni wao. Siyo mimi na hatuwezi wote kufanana, kwangu halina nafasi,” anasema na kuongeza:

“Kuna mengi ya kufanya kwa ajili ya kuboresha ndoa, hayo ndiyo yana umuhimu kwangu, ndiyo maana nimeweza kudumu kwenye ndoa kwa miaka 13 mpaka sasa, si mchezo. Si jambo dogo. Namshukuru Mungu kwa ajili ya hilo.”

AWACHANA MASTAA WASIOLEA WATOTO WAO

Baadhi ya mastaa wamekuwa na tabia ya kuwaacha watoto wao kwa wazazi wao baada ya miezi kadhaa ya kuwazaa.

Kwa upande wa Eshe, amesema halina nafasi kwake na kwamba anawashangaa sana wanawake wenzake wenye tabia hizo.

“Hiyo tabia ipo kwa wanawame wengi kwa ujumla siku hizi, lakini kwa mastaa imezidi. Mtu umemzaa mwenyewe mwanao, kwanini ukimbie jukumu la kumlea?

“Mimi namlea mwanangu mwenyewe na ninamuweka katika mazingira halisi ya Kitanzania, afuate tamaduni zetu siyo maadili ya nje. Natamani mwanangu awe na hofu ya Mungu, kwasababu hata mimi nililelewa hivyo  ndiyo sababu sijawahi kujulikana kwa skendo, najulikana kwa kazi zangu na nitaendelea hivyo,” anasema Eshe.

ANATUMIA MKOROGO?

“Baadhi ya watu hudhani labda natumia mkorogo. Hii ni rangi yangu halisi, sijawahi na wala sifikirii kutumia mkorogo. Hata kama ningekuwa mweusi sidhani kama ningetumia mkorogo kwa sababu najipenda sana, siyo mkorogo tu hata kuongeza au kupunguza chochote katika mwili wangu sifikirii kabisa.

“Nitajipamba kama mwanamke wa kisasa bila kumkosea Muumba wangu. Kwani ni nani aliyewatudanganya wanawake kuwa weupe dniyo uzuri? Tujifunze kuwa halisi, tusimkosoe Mungu,” anasema.

Mtanzania

 

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364