-->

Goodluck Gosbert Anazidi Kupasua Anga

Jina la nyota wa muziki wa Injili Nchini Goodluck Gozebert maarufu kama ‘Lollipop’ sio geni masikioni mwa wengi hasa kutokana na aina ya muziki anaoufanya.

Goodluck Gozebert

Kwa namna moja au nyingine, amechangia kwa kiasi kikubwa kubadili mahadhi ya muziki wa Injili nchini toka ule uliokuwa umezoeleka zamani na kuwa wa kizazi kipya yaani ‘Bongo Gospo’.

Ukarimu, ucheshi, heshima na nidhamu ni kati ya vitu vichache vinavyomfanya akubalike zaidi machoni pa wengi pale anapokutana nao ukiachilia mbali, kazi yake ya kiwango anayoifanya.

Mwanamuziki huyo ambaye pia ni mtunzi wa nyimbo na mtayarishaji wa muziki ameendelea kuonja mafanikio ya kipaji chake baada ya kushinda tuzo ya ‘Sauti Award’ iliyotolewa hivi karibuni nchini Marekani akishinda kipengele cha mwimbaji bora wa kiume Afrika Mashariki.

Tuzo hiyo ilitangazwa miezi minne iliyopita huku mwimbaji bora wa Afrika Mashariki wa kike, akiwa Mercy Masika wa Kenya.

Mbali na tuzo, Mwanamuziki huyo kijana ameachia video ya wimbo wake mpya unaoitwa ‘Shukrani’ ambao unaendelea kufanya vizuri kwenye vituo mbalimbali vya Luninga, redio na hata kwenye mitandao ya kijamii.

Mwananchi ilifanya mahojiano na Goodluck kuhusiana na safari yake kimuziki.

Tumaini: Hongera kwa tuzo. Watanzania watapenda kujua mchakato wa upatikanaji wake ulikuwaje?

Goodluck: Tuzo zilitangazwa miezi minne iliyopita na tuliwekwa kwenye kipengele kimoja na waimbaji wengi kutoka Afrika Mashariki.

Hii ni kama mara ya pili kwa tuzo hizi kutolewa na kipindi hiki neema ilituangukiwa Tanzania na nikashinda. Namshukuru Mungu kwa sababu sio kitu nilichopanga ila nakumbuka nilipost kuwashukuru watoaji wa tuzo huku nikiomba watu waingie kwenye mitandao na kupiga kura.

Tumaini: Unazungumziaje ujio wa kazi yako mpya?

Goodluck: Wimbo wangu mpya unaitwa ‘Shukrani’ nimeufanya chini ya mtayarishaji Mukiza.

Video imefanyika chini ya Wanene Studio Director akiwa Destro.

Wimbo huu unaashiria ujio wa albamu yangu mpya utakaokuja hivi karibuni.

Nimepata kibali na neema nyingine ya kufanya wimbo wenye mafunuo mengi.

Mfano Mungu anaweza kukuokoa kwenye ajali usijue ni yeye amefanya, unaamka kila siku asubuhi mzima na unasahau ni neema tu.

Umebahatika kuwa na kazi na unaishi vizuri kwa amani, pengine wengine uliosoma nao walipata mateso kwenye maisha yao.

Wimbo wa Shukrani utabeba albamu yangu yenye jumla ya nyimbo nane, namshukuru Mungu kwa ujio wa albamu hii.

Tumaini: Safari yako ya muziki wa injili ulianza rasmi wakati gani?

Goodluck: Safari yangu ya muziki nilianza mwaka 2005, nikiimba kwaya ya Imani ya KKKT-Mwanza na mwaka 2008 nikafanikiwa kurekodi albamu yangu.

Nilitoa albamu ‘Nimelipiwa Deni’ ikiwa na nyimbo nane na mwaka 2012 nikatoa nyingine iliyokuwa inaitwa ‘Nimeuona’ ikiwa na nyimbo nane pia.

Mwaka 2014 niliachia wimbo wa ‘Acha Waambiane’ na 2015 nikaachia wimbo wa ‘Ipo Siku’.

‘Ipo Siku’ ndilo jina la albamu yangu iliyofanya vizuri sana na ninamshukuru Mungu kwa ajili ya uwepo wa kazi hii, ambayo ndiyo ilianzisha safari yangu ya kimuziki.

Albamu hii ndiyo iliyonipatia umaarufu kama mwimbaji na ilinitambulisha vyema.

Tumaini: Hakuna safari isiyo na changamoto, kwako hii ipoje?

Goodluck: Changamoto zipo kila siku, huwa sipendi kuzizungumzia sana kwa sababu unaweza kuzisema mwingine akakata tamaa.

Mungu wetu ana nguvu kuliko changamoto na majaribu huwa yanakuja kutuimarisha.

Tumaini: Unaweza kuelezea mafanikio kwenye kazi hii ya muziki hasa kutokana na ukweli kwamba wengi wanalia hali ngumu.

Goodluck: Namshukuru Mungu kwamba kazi yangu imeweza kuwafikia wengi kuliko zile za mwanzo.

Nimekuwa nikipata mrejesho mkubwa sana juu ya nyimbo zangu na kile ambacho Mungu ameweka ndani yangu kwamba kinasaidia wengi.

Kwangu hayo ni mafanikio makubwa kwenye huduma yangu. Mafanikio ya mwilini kama nyumba, gari na nini ni ahadi ambayo Mungu alisema kama tutamtumikia kwa uaminifu atatubariki.

Najali sana mafanikio yanayoihusu huduma yangu zaidi.

Mwananchl

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364